BEKI wa kati wa Paris Saint-Germain, Thiago Emiliano da Silva, maarufu kama Thiago Silva, amemtahadharisha Zlatan Ibrahimovic kwamba kuhamia katika Premier League ni 'kujishusha'.
Silva alisema kuwa hakuna timu England unayoweza kuilinganisha na PSG, ambayo tayari imefanikiwa kushinda taji lake la nne mfululizo la Ligue 1.
"Ni rafiki yangu mzuri, lakini pia katika umri wa miaka 34 anacheza soka bora," Silva aliliambia gazeti la Mirror. "Ni mmoja wa wabora duniani, ni wa kipekee, hakuna mchezaji mwingine kama yeye."
"Kwa kweli nataka abaki PSG, siwezi kufikiria tutakavyokuwa bila yeye. Najua ana ofa kutoka England – na ni ligi kubwa – lakini sidhani kama kuna timu England ambayo ipo katika ngazi ya PSG kwa sasa. Kwangu mimi itakuwa ni kushuka kiubora kwake."
Thiago ameyasema hayo bila kujali kuwa Manchester City ya England imewang'oa wao (PSG) kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa.
Comments
Post a Comment