Kwa mara nyingine tena kijana wa kitanzania anayesukuma soka la kulipwa katika ligi ya Ubelgiji Mbwana Samatta ambaye anaitumikia klabu ya KRC Genk, alipata fursa ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo wakati kinaikabili klabu ya Club Brugge.
Hatua hiyo imekuja baada ya mwendeleo mzuri wa Samatta kwenye klabu hiyo hususan baada ya kufunga goli kwenye mchezo uliopita dhidi ya Zulte Waregem April 16 ambapo Genk ilishinda kwa magoli 2-1.
Mchezo huo ni wa pili mfululizo kwa Samatta kuanza kwenye kikosi cha kwanza lakini ukiwa ni mchezo wake wa tatu kuanza kwenye kikosi cha kwanza tangu alipojiunga na klabu ya Genk huku akiwa amesha funga magoli manne hadi sasa.
Kwenye mchezo wa leo, Genk imepata ushindi wa magoli 4-2 lakini Samatta hakufanikiwa kutumbukia wavuni katika mchezo huo. Baadaye alitolewa ikiwa ni dakika ya 76 ya mchezo na nafasi yake kuchukuliwa na Nikolaos Karelis ambaye mara nyingi wamekuwa wakipidhana.
Hiyo ni dalili nzuri kwa Samatta ambaye uwezo wake umeanza kumvutia kocha wake Peter Maes na kuanza kupewa nafasi ya kuanza katika kisi cha kwanza ndani ya miezi michache tangu atue kwenye kikosi hicho akitokea TP Mazembe.
Comments
Post a Comment