MWANDISHI na mchambuzi maarufu wa soka            raia wa Hispania, mwenye rekodi ya kuibua stori za usajili,            Guillem Balague, amesema Real Madrid iko tayari kumuuza staa            wake James Rodriguez kwa Manchester United kiangazi hiki, kama            wataweka mezani dau nono.
        Kiungo huyo mchezeshaji wa zamani wa            Monaco, amekuwa na msimu wa misukosuko Bernabeu na wiki            iliyopita alionywa na kocha wake, Zinedine Zidane baada ya            kucheka akiwa kwenye benchi wakati Madrid ikichapwa 2-0 na            Wolfsburg katika mechi ya kwanza ya robo fainali ya Champions            League.
        Staa huyo raia wa Colombia mwenye miaka            24, alichagua kuhamia kwa miamba hiyo ya La Liga akiungana na            Gareth Bale na Cristiano Ronaldo kuunda safu ya ushambuliaji            badala ya kutua Premier League baada ya kung'ara katika World            Cup in 2014.
        Kutokana na uwezo wake ina maana kwamba            licha ya kuwa na msimu mbaya, Red Devils bado wana hamu ya            kumpata staa huyo wa zamani wa Porto, na Balague ambaye            aliibua stori kubwa za usajili kama kutua kwa Angel Di Maria            Old Trafford, amesema Madrid haina tatizo na kumuuza kiangazi            hiki kama Manchester United itafika bei.
        "Ninachoweza kusema ni kwamba Real Madrid            ina zaidi ya furaha kumuuza Rodriguez… kama watapata kiasi            sahihi cha fedha," Balague aliiambia televisheni ya Sky            Sports.
        
Comments
Post a Comment