MBINU ZA STEWART HALL ZIMEFIKA MWISHO?


MBINU ZA STEWART HALL ZIMEFIKA MWISHO?

Kocha wa Azam Stewart Hall akilala mbele kuwaacha              solemba waandishi wa habari waliotaka kujua sababu za kikosi              chake kupoteza mchezo huo

Na Baraka Mbolembole

Licha ya kutokuwa na wachezaji wake wanne wa nafasi muhimu, naamini mkufunzi wa Azam FC, Muingereza, Stewart Hall alichangia kwa asilimia fulani kipigo cha 3-0 kutoka kwa Esparance ya Tunisia ambacho timu yake ilikipata katika mchezo wa marejeano wa hatua ya 16 bora katika michuano ya kombe la Shirikisho Afrika.

Kinara wa ufungaji katika michuano hiyo, Mu-ivory Coast, Kipre Tchetche mwenye magoli manne katika michezo mitatu, kiungo-mzuiaji, Mnyarwanda, Jean-Baptiste Mugiraneza, mlinzi wa kati na kiongozi wa ngome ya ulinzi, Mu-ivory Coast, Paschal Wawa na mlinzi namba mbili wa kimataifa wa Tanzania, Shomari Kapombe wote hawakuwapo katika mchezo wa usiku wa jana jijini Tunis.

Kwa mkufunzi ye yote yule kuwakosa wachezaji wake wanne muhimu kwa pamoja ni pigo lakini Hall namlaumu kwa maana alishindwa kuipanga timu yake katika usawa na kitendo cha kumuweka benchi kwa mara nyingine kiungo mkabaji wa timu ya Taifa (Taifa Stars,) Himid Mao nakitazama kama sababu kubwa ya Azam FC kuondolewa kwa mara nyingine katika hatua ya 16 bora ya michuano hiyo.

Himid alicheza kwa muda mfupi katika game ya kwanza, lakini kitendo cha nahodha huyo msaidizi kuingia tena kama mchezaji wa akiba dakika ya 79′ kilinifanya nijiulize maswali kadhaa. Je, mchezaji huyo kijana mwenye uzoefu ameshuka kiwango chake? Kama sivyo inakuaje anarudishwa benchi haraka kutoka kikosi cha kwanza?

Azam walikwenda Tunisia wakiwa tayari na 60% za kufuzu kwa hatua ya 'kapu' kutokana na ushindi wao wa 2-1 walioupata katika uwanja wa Azam Complex Chamanzi. Mbinu ya kumuanzisha Bocco kama mshambulizi pekee ilikuwa ni sahihi lakini machaguo ya nafasi ya kiungo hayakulenga timu kulinda ushindi ambao waliupata jijini Dar wiki iliyopita.

Nafikiri, Hall alipaswa kumpa nafasi ya kuanza mchezo, Himid ambaye angeweza kucheza kama kiungo mlinzi sambamba na Kipre Bolou. Machaguo ya Domayo na Salum pia yalikuwa sahihi-lakini ikimbukwe pia wachezaji hao wawili si wakabaji wazuri licha ya kwamba wanaweza pia kufanya majukumu hayo wakiwa mchezoni.

Kama, Hall alimpanga Bocco pekee kwa kutegemea mbinu ya kujilinda na kufanya mashambulizi ya kustukiza, basi hakupaswa kuanzisha viungo wanne wa mashambulizi kati ya wale watano aliowaanzisha. Ukiwatoka, Domayo na Salum sidhani kama Farid Musa ni mchezaji mwenye mbinu na uwezo wa kuzuia na kuichezesha timu, pia ni vivyo hivyo kwa Ramadhani Singano.

Wawili hawa pia si wakabaji wazuri na nafikiri kazi yao nzuri waliyoifanya katika game ya kwanza walistahili kuanza tena mchezo wa jana usiku, ila lilikuwa ni chaguo baya. Balou alianza na Jean Mugiraneza kama viungo wakabaji na wapandishaji timu katika game ya wiki iliyopita na timu ilionekana kuwa na nguvu katikati ya uwanja hata pale walipokuwa wakishambuliwa. Domayo, Bolou, Salum, Singano na Farid walicheza vizuri katika dakika 45′ za mchezo wa jana na timu ilipeleka mashambulizi kadhaa lango mwa Esperance.

Lakini kila waliposhambuliwa beki ilionekana kupoteza mwelekeo. Shukrani kwa golikipa kijana, Aishi Manula ni nguzo/mlingoti wa magoli. Erasto Nyoni, Wazir Salum, David Mwantika walianza katika ngome isiyo na mchezaji ye yote wa kigeni na kosa lao la kwanza kubwa lilifanywa na Mwantika dakika ya 46′ baada ya kumuangusha Ben Youssef nje kidogo ya eneo la hatari na kuzaa mkwaju uliokufa.

Esperance kama ilivyo kwa timu nyingi za Kiarabu wakatumia nafasi hiyo kufunga goli lao la kwanza katika mchezo huo huku likiwa la kusazisha katika matokeo ya jumla ( 2-2.) Baada ya kufungwa goli hilo Azam wakaanza kupoteza uelekeo na mbinu yao ya kucheza kwa kujilinda ikavurugwa dakika ya pili tu baada ya kuanza kwa kipindi cha pili. Dakika ya 63′ wakaruhusu goli la pili na kufikia dakika ya 79′ walikuwa nyuma 3-0 (4-2 matokeo ya jumla.)

Hall ni kocha mzuri lakini huwa hana mbinu sahihi katika game muhimu. Tangu wakati ule alipofeli, Rabat (2013) hajawahi kuwa makini na machaguo muhimu ya wachezaji katika kikosi chake kila nyakati muhimu. Azam FC imetolewa tena hatua ya 16 bora. Michuano yao minne ya CAF wameshindwa kushinda ugenini na kupoteza matokeo yao ya ushindi katika uwanja wa nyumbani.

2013 timu haikuwa na uzoefu, 2014 timu iliathiriwa na uwanja mbovu kule Msumbiji, 2015 timu ilikuwa ikicheza klabu bingwa Afrika kwa mara ya kwanza, 2016 (ikicheza kwa mara ya tatu michuano ya shirikisho) Azam FC imeangushwa na uwezo mdogo wa kimbinu na kiufundi wa kocha Stewart Hall.

Ni wazi sasa timu hiyo haipaswi kulia kuhusu uzoefu bali wanahitaji mkufunzi bora mwenye ufahamu na soka la Afrika kama Mnigeria, Stephen Keshi au Daniel Amokachi. Hall amefikia mwisho wa mbinu zake katika kuindeleza timu hiyo ndani ya uwanja.

Sasa ni wakati mwafaka wa Stephen Keshi kuipaisha Azam FC katika malengo yao ya kimataifa. Wampe timu Keshi kwani wanao uwezo wa kumlipa chochote. 'Mbinu za Hall zimefikia mwisho, Azam FC inamuhitaji Stephen Keshi sasa.

Katika moja ya comment za mchangiaji mmoja katika ukurasa wangu wa facebook (Nolas Jose) baada ya mimi kuposti matokeo ya game ya Esperance 3-0 Azam alisema: "Duh!! Nimesikitishwa sana kwa matokeo ya Azam kupoteza Mechi. Lakini pia ni vizuri tuangalie tunapojikwaa, na sio tunapoangukia. Katumbi (mmiliki wa TP Mazembe) huwa anasajili wachezaji wa maana (majembe kweli) ili kushindana na Club kubwa barani Afrika kama Al Ahly (Misri) Esperrance (Tunisia) Enyimba (Nigeria) Raja Cassablanca (Morrcco) nk."

"Tofauti na viongozi wa timu zetu hizi, haswa hizi kongwe (kwa historia) na siyo kubwa (kwa mafanikio) usajili wao mara nyingi siuelewielewi! Nikianza na usajili wa wachezaji wa nje, Wachezaji tunaoletewa wengine viwango vyao afadhali ya wazawa. NB: hata kwenye timu zao za Taifa hawamo (TFF) waliagiza hilo lizingatiwe, sijui limeishia wapi!! "

"Sasa hapa tatizo uhaba wa pesa au ndiyo mambo yetu yale ya 10%? Nikirudi kwenye usajili wa wachezaji wa ndani, hapa ni kichekesho kidogo. Uongozi unasajili mchezaji (Mara chache sana hushirikiana na benchi la ufundi) Kwa sababu tu, kule kwenye timu yake anafanya vizuri na si mahitaji ya timu kwa nafasi anayocheza mchezaji husika, maana utashangaa wana wachezaji wa aina hiyo wa nne, tano hadi sita!!".

"Hapa kuna vitu viwili. 1. Kuidhoofisha timu pinzani maana huyo mchezaji/wachezaji huwa wanasumbua timu hizo zinapokutana kwenye Mechi. 2. Viongozi kuwaaminisha wanachama /wapenzi wa hizo timu kuwa "wapo kikazi kweli maana wamechukua jembe kutoka timu pinzani!!"

"Kila mwaka tunabadilishana wachezaji hapahapa tu 'kama stick za pooltable' maendeleo ya soka hakuna! Nasema haya ni mawazo mgando, kila siku kusajili kwaajili ya kufungana /kushindana sisi kwa sisi! Ukitaka kufanikiwa, shindana na aliye Juu yako na si ulienae sawa au wa chini yako maana hapo utakuwa unapiga hatua kurudi nyuma (inatakiwa umakini kulielewa hili)"

"Viongozi msajili wachezaji watakaoweza kushindana na timu kubwa kama TP Mazembe nk. Siyo mnasajili ili Simba kumfunga Yanga/Yanga kumfunga Simba, hizi timu 'level' yake ni moja ni sawa na kupiga hatua kurudi nyuma."



Comments