MAURICIO Pochettino "anawapasua kichwa" mabosi wa Tottenham kutokana na kuchelewa kusaini mkataba mpya.
Spurs inataka kumalizana haraka na kocha huyo kutokana na hofu kuwa anaweza kwenda Manchester United baada ya Paris Saint-Germain kujiunga katika kumuwinda Jose Mourinho anayetarajiwa kumrithi Louis van Gaal kiangazi hiki.
Barcelona na Real Madrid nazo pia zinatajwa kummezea mate kocha huyo baada ya kuibadili Spurs kuwa timu ya kutisha Ulaya katika kipindi cha misimu miwili.
Spurs wamekuwa wakimsubiri kwa wiki kadhaa sasa Pochettino kutia saini mkataba wa miaka mitano wenye thamani ya pauni milioni 5 na bonasi.
Pochettino ambaye bado ana zaidi ya miaka mitatu katika mkataba wake wa sasa aliosaini mwaka 2014, alisema mwezi huu kuwa anataka kubaki Spurs.
Lakini akasema hana muda wa kujadili mkataba kwa sasa, kwa sababu hataki "kuvurugwa" katika harakati zake za kuipa Spurs taji la kwanza tangu 1961.
Hata hivyo, mabosi wa klabu hiyo wanaamini Pochettino mwenye umri wa miaka 44, ana uwezekano wa kusaini mkataba, lakini wakakiri kuwa kuchelewa kwake kunawaweka katika hali ya wasiwasi.
Comments
Post a Comment