MASHUJAA WATATU USIKU WA MABINGWA ULAYA


MASHUJAA WATATU USIKU WA MABINGWA ULAYA

img_5807.jpg

Na Athumani Adam

Timu ambazo zitacheza hatua ya nusu fainali, klabu bingwa Ulaya maarufu kama UEFA Champion League tayari zimejulikana. Baada ya mechi za Jumanne na Jumatano wiki hii kuchezwa, tumeona Manchester City ya Uingereza, Real Madrid na Atletico Madrid za Hispania na Bayern Munich ya Ujerumani zikisonga mbele.

Kama ilivyo kawaida, kila kwenye pambano huibuka shujaa. Hivyo kutokana na mechi za raundi ya pili hatua ya robo fainali kuchezwa kuna watu ambao wamefanya vizuri sana kuzisaidia timu zao kupata mafanikio na kuvuka kuelekea hatua inayofuata.

Napenda nikupe watu watatu ambao kwa mtazamo wangu walikuwa na mchango mkubwa kuzisaidia timu zao kushinda mechi za juzi na jana. Kama ingekuwa ni filamu basi ningesema hawa ni 'ma-sterling' wa usiku wa Ulaya yaani 'European Night'.

  1. Joe Hart Manchester City vs PSG)

Joe Hart 1

Huyu ni kipa wa Man City, pia alikuwa naodha wa timu hiyo kwenye usiku wa Jumanne. Muingereza huyu pekee kwenye kikosi cha kwanza cha City niliona mchango wake mkubwa kwenye mechi dhidi ya PSG usiku wa Jumanne  pale uwanja wa Etihad jijini Manchester.

Kama Hart angecheza chi ya kiwango kile, yawezekana City wangepoteza mechi ile. Alifanya kazi kubwa kuondoa hatari ambazo kwa asilimia 90 zilikuwa zinazaa magoli. Hebu kumbuka zile free-kicks mbili za Zlatan Ibrahimovic zilivyochezwa kiufundi sana na Hart.

Kisha akaondoa tena mpira wa kichwa wa beki raia wa Brazili, Thiago Silva ambao ulitokana na kona. Ingawa Kevin De Bruyne alifanya vyema, mabeki kina Otamendi na Mangala walikuwa vizuri pia, kwangu shujaa alikuwa wa mchezo alikuwa ni Joe Hart.

  1. Cristiano Ronaldo (Real Madrid vs Wolvesburg)

Cristiano vs Wolfsburg

Real Madrid walipoteza mchezo wa kwanza, wiki moja iliyopita kule Ujerumani. Ilikuwa dhidi ya Wolvesburg wakalala 2-0 huku wapenzi wengi wa soka wasiamini kilichotokea.

Mambo yakawa tofauti pale Bernabeu, kwenye mechi ya marudiano usiku wa Jumanne. Ni Cristiano Ronaldo ndiye aliyepindua matokeo kwa hat-trick ya juzi usiku, Madrid wakapata ushindi wa 3-0 pia wakapita kwenda hatua inayofuata kwa uwiano wa mabao yaani 'aggregate' 3-2 baada ya mechi zote mbili. Binafsi Ronaldo alikuwa shujaa pia ndani ya Stantiago Bernabeu.

  1. Diego Simeone (Atletico Madrid vs Barcelona)Simeone

Huyu ni kocha mpambanaji wa Atletico Madrid ya Hispania, ana kila taji la ngazi ya klabu isipokuwa ubingwa wa UEFA Champion League. Namuweka Simeone kwenye mashujaa wangu watatu kwa sababu moja, mbinu zake zimesaidia kuwang'oa mabingwa watetezi wa mashindano haya FC Barcelona baada ya ushindi wa 2-0 nyumbani.

Baada ya kupoteza mchezo wa awali 2-1 pale Camp Nou huku wakiwa pungufu kukotana na kadi nyekundu aliyopewa mshambuliaji, Fernando Torres jana Atletico chini ya Simeone waliwathibiti Barca wakadhibitika. Si kazi rahisi kucheza na Barca halafu wasitikise nyavu zako hata mara moja.

Pia Simeone alikuwa zaidi ya muhamasishaji usiku ule, kwa mashabiki wake pamoja na wachezaji wake. Alikuwa anafanya kazi mbili kwanza kutoa maelekezo pili kuamsha jukwaa lishangilie muda wote. Kwa kazi ambayo aliifanya usiku ule wa UEFA acha nimuweke kwenye orodha hii.



Comments