MANCHESTER CITY            ilitarajiwa kuweka mezani pauni milioni 80 kwa ajili ya            kumrejesha England staa wa Juventus, Paul Pogba kiangazi hiki,            lakini sasa haina tena mpango nae na badala yake inamtaka            Alvaro Morata.
        Gazeti la The Sun            limedai kuwa City kwa sasa inaelekeza nguvu zake katika            kumtwaa Morata – pia wa Juventus ili kuiongezea makali safu            yake ya ushambuliaji.
        Straika huyo wa            kimataifa wa Hispania, amefunga mabao sita tu na kupika sita            katika mechi 31 za Serie A msimu huu, huku zaidi ya nusu            akifunga akitokea benchi kutokana na kukabiliwa upinzani wa            namba kutoka kwa Simone Zaza na Paolo Dybala.
        Licha ya kuwa Arsenal            imekuwa ikimtamani kwa muda mrefu Morata mwenye miaka 23 na            kutaka kumsajili kiangazi hiki, mtandao wa CalcioMercato            umeripoti kwamba kocha ajaye Chelsea, Antonio Conte pia ni            shabiki mkubwa wa straika huyo.
        Kutokana na timu tatu            za Premier League kuonyesha nia ya kumtaka straika huyo, Real            Madrid inaonekana kujipanga kumnunua na kisha kumuuza kwa            faida.
          
          
                                        Morata aliondoka Madrid            mwaka 2014, lakini klabu hiyo ya Hispania ina ubavu wa            kumrejesha kwa pauni milioni 23.7 kulingana na mkataba            walioingia na Juve.
        
Comments
Post a Comment