MAMBO KUMI NILIYOJIFUNZA BAADA YA ROBO FAINALI UEFA CHAMPIONS LEAGUE


MAMBO KUMI NILIYOJIFUNZA BAADA YA ROBO FAINALI UEFA CHAMPIONS LEAGUE

uefa

  1. Inawezekana kabisa watu na wachambuzi mbalimbali wamesahau kama kuna mchezaji bora anayeitwa Koke. Ni nadra sana kukutana na mchezaji bora anayeishi maisha ya ukimya kama huyu, lakini huyu ndiye hasa anayeleta mlinganyo unaotakiwa ndani ya mfumo wa Simeone na kuweka usawa baina ya ushambuliaji na ulinzi. Ni ngumu kuzuia mbinu za Atletico kama akiwa katika kiwango chake, hata Barcelona walishindwa hilo.
  1. Ni ngumu sana kuhesabu vipaji vya Atletico vikatokea vya kukustua ambavyo vingeweza kujaza kiganja cha mtoto mchanga. Lakini Diego Simeone anaonyesha kuwa soka la kisasa mfumo na mbinu ndio unaoamua kila kitu. Sio kila siku vipaji vitashinda, kuna nyakati nyingi za shida ambazo zinahitaji nguvu na juhudi. Katika hili unaweza kuwaweka Leicester wa Ranieri.
  1. Ukimtizama De Bryune anachofanya, kisha usiku unaofuata ukatizama miguu ya Julian Drexler na wakati huohuo ukaziweka mboni zako mahala ambapo Antoinne Griezman yupo unaweza kuamini kuwa hawa ni moja ya wachezaji bora duniani. Lakini ubongo wako lazima ubadilike haraka sana pindi ukishuhudia anachofanya Ronaldo kisha ukawaza anachoweza kufanya Messi. Umefika muda nikatamani Messi na Ronaldo wangekuwa na umri wa Ronaldinho, huko wangepambana na mafahari wenzao, vinginevyo vipaji hivi havitatwaa tuzo mpaka vistaafu.
  1. Pep anatuongopea uongo uliokuwa kweli. Guardiola anatudanganya, na anatudanganya uongo wa kweli. Guardiola hana watu sahihi katika eneo la ulinzi na hana uhakika mpaka sasa yupi anaelewana na yupi kati ya viungo anaowajaribu. Ni uongo wa kweli kwa sababu anaendelea kuchanja mbunga huku wengi wakiendelea kumuhofia. Huu uongo unaweza kugeuka ukweli kabisa kwa sababu ya kitu kinaitwa fear factor of the opponent. Benfica wangeweza kumwondoa, Juventus walitakiwa kumwondoa lakini kwa sababu ni mjanja, uongo wake utaendelea kuaminika, na mwisho Kobe atashinda mbio ndefu.
  1. Mlimwona Wenger mwehu aliposema Barcelona na MSN wanakabika? Zidane na Simeone walimsikiliza vyema sana. Ukitaka kuwazuia Barcelona hawa wa sasa, waachie mpira kisha zuia kuanzia kwenye nusu. Kwa sababu hawana tena Xavi itambidi Busquet asogee kupiga pasi nyingi, ili kumpunguzia presha Messi anasogea chini sana kupokea Mipira, Neymar anaenda pembeni zaidi kupanua nafasi, jambo linalofanya Suarez ajitenge. Ikishafikia hapa kaba kwa nguvu kisha kimbia ukipokonya mpira, utawafunga kila siku. Tatizo kwa Wenger alikosa wazuiaji sahihi, kisha akakosa Ronaldo ama nusu yake ambaye ni aina ya kina Griezman.
  1. Udhaifu wa kwanza wa PSG ni uwanja wao wa nyumbani kisha Zlatan Ibrahimovic. Hawajawahi kuwa na nidhamu katika uwanja wao wa nyumbani kitu ambacho ni silaha kubwa kwenye UEFA lakini anayewafungia hesabu ni Zlatan Ibrahimovic. Sina kumbukumbu mara ya mwisho lini amekuwa chachu ya ushindi hasa wa PSG katika michezo mikubwa. Umefika wakati wa PSG bila Zlatan Ibrahimovic maana kuna wakati kiungo chako muhimu hata kama ni kichwa ndio kikawa chanzo cha kuachika.
  1. Utafiti wa tiba haujawahi kufanyika kabla ya ugonjwa kulipuka lakini Perez na Madrid waliamua kwa makusudi kuukana utafiti uliokuwa tayari na thabiti. Walau Zidane alifanya utafiti wake wa kibubu na kumwingiza Casemiro ndani ya kikosi. Kama Perez hapendi wanaume wenye sura ngumu, walau huyu anaweza kuwa handsome anayefanya kazi za kibabe na anasababisha walau watu wagundue kwanini Kroos na Modric wanastahili kuwa Madrid. Zidane mjanja sana.
  1. Moyo unaniambia Manchester City wanaweza kuwa kifurushi cha kustukiza msimu huu wa UEFA, lakini akili inanikumbusha kuwa Yaya Toure amepona. Yaya Toure alikuwa kiungo bora aina ya box to box, lakini sina hakika kama kwa sasa anaweza kucheza kutoka duara moja kwenda jingine kwa ufasaha kwa dakika 90. Huyu ndiye anayeweza kuwapa ubora zaidi kwa maana ya uzoefu wa Uefa ama kuwaua. Sijaiona Man City ikicheza vyema akiwa ndani, binafsi asingeanza mechi zinazofuata. Huyu ni dawa kama ataamua kuiua misuli yake inayochoka lakini ni gonjwa kama akihifadhi, itategemea na Man City watamtumiaje. Mi nampachika kuwa X Factor wa safari yao.
  1. Kumtizama Fellaini ndani ya Old Trafford kisha ukagundua kuna kijana anaitwa Renato Sanchez anatafuta malisho kule Benfica, moyo wako utachuruzika machozi yenye chumvi mwisho ukaitesa damu yako. Watu wengi hawajamtizama vyema lakini anaweza kuwa miongoni mwa wachezaji watakaoitikisa dunia siku zijazo. Tatizo la soka ni kama ujauzito, huna uhakika kama mama atajifungua salama, lakini kuna haja ya kumwiba kiongozi wa Scouting wa benfica.
  1. Natafakari kinachoweza kuwa kichwani mwa Zidane kwa sasa. Ana bomu lake linaitwa Ronaldo, ana bunduki yake nzito inaitwa Bale kisha anajiona amepata ngao inaitwa Casemiro. Akitizama kushoto kulia hawezi kuwahitaji Atletico Muda huu, hawa anaweza kuwaadhibu vyema tu wakiwa wote ugenini kule San Siro kwenye fainali. Bayern Munich na safu yao ya ulinzi anawahimili, Man City anawaweza. Ndoto zake kwa sasa zinaweza kuwa amevaa medali na Ronaldo ametwaa Ballon D'OR maana hakutakuwa na sababu ya kumnyima.

Ahsanteni.

By Nicasius Nicholaus Agwanda (Coutinho Suso)



Comments