UNAJUA kama beki wa kushoto wa Bayern Munich, David Alaba (pichani kulia) ndoto yake ni kuichezea Arsenal? Basi habari ndiyo hiyo, na alitaka kujiunga na klabu hiyo tangu siku za awali za maisha yake ya soka.
Kwa mujibu wa mwandishi raia wa Australia, Andras Heidenreich aliyeandika katika jarida la France Football wiki hii, Alaba mwenye umri wa miaka 23, ambaye ni mmoja wa mabeki wa kiwango cha juu duniani, alikuwa shabiki mkubwa wa the Gunners na hasa Patrick Vieira.
Akiandika jinsi Bayern walivyomnasa Alaba, alisema: "David alikuwa vizuri kiasi kwamba Austria (Wien) haikuweza kuendelea nae. Heiko Vogel, kocha wa kikosi cha U14 cha Bayern, alimuona wakati wa mashindano mjini Bremen. Moja kwa moja alivutiwa na kipaji chake na kujitoa kwake uwanjani.
"Alikuwa bora katika timu yake pamoja na (Christoph) Knasmullner. Hata hivyo, David hakusema mara mbili kwa Bayern Munich, timu ambayo hakuihusudu. Alipendelea Arsenal, ambako kioo chake, Patrick Vieira, alikuwa akicheza."
Mapenzi ya Alaba kwa Arsenal si siri, na mwenyewe huko nyuma mwaka 2009 alikiri kwamba angalipenda kuichezea timu hiyo ya London Kaskazini, licha kwamba inaonekana kuwapo uwezekano mdogo kwa sasa baada ya kupata mafanikio makubwa katika Bundesliga.
Staa huyo wa kimataifa wa Austria, ameshinda mataji manne ya Bundesliga na Champions League akiwa Allianz Arena, akiwa sehemu ya kikosi kilichobeba mataji matatu kwa mpigo msimu wa 2012/13.
Hivi karibuni Alaba alisaini mkataba mpya wa miaka mitano Bayern Munich utakaomweka hadi mwaka 2021.
Comments
Post a Comment