STAA wa zamani wa Chelsea, Didier Drogba, amesema atalistaki gazeti la Daily Mail kwa kuandika habari za uongo dhidi yake na kumchafulia jina lake.
Drogba amefikia hatua hiyo baada ya Daily Mail kuchapisha habari zinazodai kwamba anatumia chini ya asilimia moja ya fedha anazokusanya kupitia mfuko wake wa kusaidia jamii, kutimiza lengo hilo.
Gazeti hilo limesema ni pauni 14,115 pekee kati ya milioni 1.7 zinazotolewa na wachezaji nyota na wafanyabiashara zinazotumika kusaidia watoto Afrika.
"Hakuna ulaghai, hakuna ufisadi na hakuna udanganyifu," ilisema taarifa ya Drogba mwenye umri wa miaka 38.
Drogba, raia wa Ivory Coast ambaye kwa sasa anaichezea Montreal Impact ya Canada, amelishutumu Daily Mail kwa kuweka hatarini maisha ya maelfu ya watoto wa Afrika.
Kutokana na taarifa hiyo ya Daily Mail, tume inayodhibiti mashirika ya kusaidia jamii yaliyosajiliwa Uingereza, imesema inachunguza madai ya ukiukaji wa sheria.
Comments
Post a Comment