BAADA ya Leicester City kuichapa Swansea 4-0 na kujiimarisha kileleni mwa Ligi Kuu ya England, kocha CLAUDIO RANIERI amesema sasa mawazo yake yote ni katika kutwaa taji la Premier League.
Huo unakuwa ni ushindi wa kwanza mkubwa kwa Leicester tangu msimu huu uanze. Mara ya mwisho klabu hiyo kuvuna ushindi mnono ilikuwa ni katika mechi ya mwisho ya msimu uliopita dhidi ya Queens Park Rangers ambapo iliibuka na ushindi wa 5-1.
Leicester inaongoza ligi ikiwa na pointi nane zaidi ya Tottenham Hotspur iliyo nafasi ya pili wakati zikibaki mechi nne kumaliza msimu.
Ranieri hajawahi kukiri huko nyuma kama kikosi chake kipo katika nafasi ya kutwaa ubingwa, lakini anakubali kuwa lazima wabaki katika kiwango chao walichokionyesha katika mchezo dhidu ya Swansea Jumapili ili kumamilisha njozi yao ya kutwaa taji la Premier League.
Akizungumzia mechi dhidi ya Swans, Ranieri alisema walifanya maamuzi kadhaa katika kuunda kikosi chake cha kwanza wakati straika wake nyota, Jamie Vardy akiwa amesimamishwa kucheza mechi mbili.
"Tulibadili kitu fulani. Bila Jamie Vardy tukaweza kufanya mkakati mwingine na ukazaa matunda makubwa.
"Wakati unapotaka kushinda taji ni muhimu kushinda kila mechi. Swansea ni ngumu na inacheza vizuri lakini tulipambana na kushinda mechi kwa sababu tunataka kushinda taji la Premier League".
Mbadala wa Jamie Vardy, Jose Leonardo Ulloa akafunga mara mbili dakika ya 30 na 60 huku kiungo mshabuliaji Riyad Mahrez akitupia bao la kwanza dakika ya 10 wakati Marc Albrighton alihitimisha karamu ya magoli dakika ya 85.
Comments
Post a Comment