KAMA ulitazama mechi ya awali ya nusu            fainali ya Champions League kati ya Atletico Madrid na Bayern            Munich iliyopigwa Estadio Vicente Calderon Jumatano usiku,            hautapata kigugumizi kukiri kuwa Augusto Fernandez ndiye            aliyerahisisha ushindi kwa wenyeji.
        Kiungo huyo wa ulinzi raia wa Argentina            aliyeanzishwa na Diego Simeone badala ya Yannick Ferreira            Carrasco, alikuwa msaada mkubwa katika kuibana Bayern Munich            hadi ikashindwa kuwa na ufanisi katika eneo la kiungo.
        Augusto alipiga pasi zake kwa ukamilifu wa            asilimia 84, akidhihirisha kwamba anaweza pia kusambaza mpira            kwa wenzake kama kiungo wa ulinzi, na alikamata nafasi ya pili            nyuma ya Koke kwa kukimbia kilomita nyingi dimbani – kilomita            12.4.
        Staa huyo alifanya kazi muda wote dimbani,            na kuiwezesha Atletico kumaliza dakika 90 nyumbani Calderon            bila nyavu zake kutikiswa kuelekea mechi ya marudiano Allianz            Arena.
        Kama Simeone ataamua kumwamini tena            Augusto, na akafanikiwa kuwa kwenye kiwango cha juu kwa mara            nyingine, Bayern Munich watakuwa na wakati mgumu kuweza            kugeuza matokeo mechi ya marudiano Jumanne ijayo.
        
Comments
Post a Comment