MMILIKI wa Chelsea, Bilionea Roman Abramovich, amejipanga kuandika rekodi ya dunia ya uhamisho kwa kumsajili kiungo nyota wa Juventus, Paul Pogba kiangazi hiki.
Mwanzoni mwa wiki hii, Chelsea ilimtangaza Antonio Conte kuchukua nafasi ya kocha wake wa muda, Guus Hiddink baada ya fainali za Euro 2016 na Mtaliano huyo anataka kuungana na nyota huyo wa timu yake ya zamani ya Juve aliyoipa taji la Serie A mara tatu kabla ya kupewa kibarua cha kuinoa timu ya taifa ya Italia.
Mtandao wa The Sun unasema kuwa Abramovich sasa yu tayari kufikia dau la pauni milioni 97 linalotakiwa na Juve kuweza kukamilisha uhamisho wa supastaa huyo Mfaransa mwenye umri wa miaka 23.
Ili kuhakikisha inafanikiwa dili hilo, inaelezwa kuwa Chelsea imeamua kuachana na straika wa Paris Saint-Germain, Edinson Cavani anayetakiwa pia na Juventus ili kujenga mahusiano mazuri na miamba hiyo ya Italia.
Comments
Post a Comment