Magoli mawili kutoka kwa Danny Lyanga na HamisI Kiiza yameipa Simba ushindi wa tatu kwenye uwanja wa Mkwakwani msimu huu na kuondoka na pointi zote tisa kwa kuzifunga timu za Tanga kwenye uwanja wa Mkwakwani na kuendelea kutamalaki kileleni mwa ligi na sasa imefikisha jumla ya pointi 57 baada ya kucheza michezo 24 ya ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara.
Mchezo hakuwa rahisi kwa Simba licha ya kuibuka na ushindi wa magoli 2-0 mbele ya Coastal Union ambayo inakamata mkia kwenye ligi kutokana na kukumbana na upinzani mkali kutoka kwa 'wagosi wa kaya' ambao walishindwa kupata mabao licha ya kupata nafasi kadhaa za kufunga.
Danny Lyanga aliifungia Simba goli la kwanza dakika ya 39 kipindi cha kwanza kisha Kiiza akamaliza kazi dakika ya 51 na kupeleka shangwe kwenye mtaa wa Msimbazi.
Takwimu na rekodi muhimu
- Simba imezifunga timu zote za Tanga kwenye uwanja wa Mkwakwani msimu huu ikianza kushinda kwa bao 1-0 mechi yake ya ufunguzi wa ligi dhidi ya African Sports kisha kuifunga Mgambo JKT na kumaliza na Coastal Union.
- Simba imepata pointi 6 dhidi ya Coastal Union msimu huu baada ya kushinda mechi zote mbili za ligi dhidi ya timu hiyo ya Tanga, Simba iliifunga Coastal kwenye mchezo wa awali kwenye uwanja wa taifa kisha leo kwenye uwanja wa Mkwakwani.
- Wachezaji watatu wa zamani wa Simba wanaocheza Coastal Union walikuwa wakikutana na timu yao ya zamani (Abdulahim Humoud, Ibrahim Twaha na Ally Shiboli.
- Kocha wa Simba Jackson Mayanja alikuwa anakutana na Coastal Union kwa mara ya kwanza tangu aondoke baada ya kuchukuliwa na Simba. Mayanja ameiongoza Simba kushinda mechi 10 kati ya 11 za ligi
- Hamisi Kiiza amefunga bao lake la 19 kwenye ligi msimu huu na kumwacha mpinzani wake wa karibu Amis Tambwe kwa magoli mawili.
- Simba sasa inaongoza ligi kwa tofauti ya pointi saba dhidi ya wapinzani wake kwenye mbio za ubingwa Yanga na Azam zenye pointi 50 kila moja huku zikiwa zimecheza mechi 21 mechi tatu nyuma ya Simba.
Comments
Post a Comment