Roy Keane amedai kwamba Arsene Wenger ana kundi kubwa la wachezaji ambao wengi wao ni dhaifu na kuwashutumu wachezaji wa Arsenal kuwadanganya mashabiki wao.
Arsenal jana ilitupwa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Barcelona kwenye uwaja wa Camp Nou.
Vile vile wametupwa nje ya michuano ya FA baada ya kufungwa na Watford Jumapili iliyopita huku wakikabiliwa na shughuli pevu ya kupunguza pengo la alama 11 dhidi ya vinara wa ligi Leicester ambao wanapewa nafasi kubwa ya kutwaa ndoo ya EPL msimu huu.
"Hii inadhihirisha kuwa wana wachezaji wengi ambao ni dhaifu ambao kwenye baadhi ya michezo yenye uzito hawana msaada wowote," nahodha huyo wa zamani wa Man United aliiambia ITV.
"Hakuna shaka kwamba presha ya mashabiki kwa miezi ya hivi karibuni imewayumbisha sana, sasa kama huwezi kustahimili presha ya mashabiki basi haupaswi kuwa pale", aliongeza.
"Inavyoonekana dhahma ilikuwa tayari ilishafanyika kwenye mchezo wa awali. Sidhani kama kuna aibu kubwa baada ya kupoteza kwa idadi ya magoli 3-1 juhudi zimeonekana – lakini nadhani Barcelona walijua jinsi gani ya kuwadhibiti", alimalizia.
Comments
Post a Comment