MSHAMBULIAJI wa Borussia Dortmund, Pierre-Emerick Aubameyang, anayetolewa macho na timu za Premier League na Ligue 1, amefanya mahojiano na televisheni ya BeIN Sports na kusema kuwa alimuahidi babu yake kwamba siku moja angelipenda kucheza soka Hispania.
Akizungumza katika kipindi cha Club de Dimanche, mshambuliaji huyo raia wa Gabon aliyeshinda tuzo ya mwanasoka bora wa mwaka Afrika mwaka jana, alisema: "PSG? Hilo si lengo langu. Siwezi kusema kitu kingine chochote kuhusu hilo. Sioni sababu yoyote ya kurudi Ufaransa ambako niliondoka miaka mitatu iliyopita.
"Real Madrid? Hakuna makubaliano lakini… Nilimuahidi babu yangu ningalipenda kucheza huko siku moja. Kwanini nisitake kuvumbua mambo mapya? Kama nilivyosema mara kadhaa, nimgependa kucheza Hispania na kuna hali nzuri ya hewa kwa mara moja katika maisha yangu [kicheko]…"
Dortmund inamthaminisha Aubameyang kwa euro milioni 100, bei ambayo Real Madrid inaweza kukaa chini kuijadili ili kumpata staa huyo aliyesaini mkataba wa kukaa Westfalenstadion hadi 2020.
Zinedine Zidane ni mpenzi mkubwa wa staa huyo mzaliwa wa Ufaransa, mwenye miaka 26, ambaye amepiga mabao 33 katika mechi 39 msimu huu.
Akiwa Ufaransa, aliwahi kuzichezea Dijon, Lille, Monaco na Saint-Étienne.
Comments
Post a Comment