NANI KUNUNUA NAMBA 45 MSIMU WA USAJILI MAJIRA YA KIANGAZI



NANI KUNUNUA NAMBA 45 MSIMU WA USAJILI MAJIRA YA KIANGAZI

MILAN, ITALY - FEBRUARY 03: Mario Balotelli of AC Milan              #45 walks on the pitch during the Serie A match between AC              Milan and Udinese Calcio at San Siro Stadium on February 3,              2013 in Milan, Italy. (Photo by Claudio Villa/Getty Images)

Na Athumani Adam

Mwanafalsafa wa lugha ya kiingereza, William Shakespear aliwahi kusema "we know where we are, but know not where we may be". Shakespear alimaanisha kwamba "tunajua tulipo sasa lakini hatujui wapi tutakuwepo".

Ligi nyingi za mataifa makubwa barani Ulaya zipo ukingoni msimu wa 2015/16, kabla ya kumalizika miezi miwili ijayo, wapo wachezaji watakaoenda Euro 2016 kule nchini Ufaransa kuwakilisha mataifa yao. Pia wale ambao mataifa yao hayajafuzu Euro pamoja na wale wachezaji wa mabara mengine watakuwa sehemu mbali mbali kwa mapumziko baada ya msimu.

Kama alivyosema Shakespear hatujui wapi tutakuwepo baadaye, kauli hii inawagusa baadhi ya wachezaji ambao hawana uhakika wa kwenda na timu zao kwenye Euro 2016 kule Paris, yawezekana kutokana na sababu mbalimbali ikiwepo kushuka viwango kwenye vilabu vyao.

Bila shaka kauli hii ya Shakespear inamgusa mshambuliaji wa AC Milan, Super Mario Balotelli. Balotelli amekuwa na kiwango duni ndani ya kikosi cha Milan, tena hapewi muda mwingi wa kucheza baada ya kutoka kwenye operasheni aliyofanyiwa mwezi November.

Hali hii inatia mashaka kwa mtukutu Balotelli kwenda na Azzuri kwenye michuano ya Euro chini ya Conte kule Paris. Vile vile hatma ya Balotelli kwenye msimu wa majira ya kiangazi wakati wa usajili bado ngumu kubashiri.

Kutokana na kiwango chake kipindi hiki si rahisi kwa AC Milan ambayo inatafuta kurudisha heshima yake ya zamani barani Ulaya kumbakisha Balotelli. Pia itakuwa ngumu kurudi kwenye klabu yake ya Liverpool ambayo imempeleka Balotteli kwenye klabu ya AC Milan kwa mkopo.

Binafsi kuna wasiwasi mkubwa wa kumpoteza Balotelli kwenye soka la Ulaya akiwa na umri mdogo wa miaka 25. Tunaelekea kumpoteza mchezaji mwenye kipaji kutokana na tabia yake ya kucheza kwa kutojituma sana uwanjani. Amefanya hivyo akiwa Inter Milan, Man City hata alivyorudi Liverpool baada ya kwenda AC Milan msimu wa 2013/14.

Kwa sasa hapati nafasi mbele ya Carlos Bacca, Luis Andriano na M'baye Niang pale Milan. Pia sidhani kama akirudi Liverpool kuna uwezekano wa kupata nafasi mbele ya kina Orig, Benteke wala Dani Starrudge.

Pia hana uhakika wa kwenda Paris chini Conte mbele ya kina Stephano El- Sharrawy, Graziano Pelle na Simon Zaza.

Balotelli alibebwa mara mbili na baba yake wa mpira, Roberto Mancini pale Inter Milan na baadaye akamvuta Man City lakini  akaamua kumpiga mateke aliyembeba, akaishia kugomabananae mazoezini. Uwezo wake pamoja na tabia yake bila shaka tutampoteza mapema barani Ulaya.

Inasikitisha kuona mchezaji aliyefanya vizuri Euro 2012 kule Poland na Ukraine kwa kuwaadhibu Ujerumani kwa mabao mawili maridadi mechi ya nusu fainali kashuka kiwango miaka minne baadaye.

Sijui anaeleka wapi majira ya kiangazi akiwa na namba 45 yake mgogoni , tusubiri tuone.



Comments