MTAZAMO WANGU: ‘MSN’ KUUSAMBARATISHA MZIMU WA CHAMPIONS LEAGUE…


MTAZAMO WANGU: 'MSN' KUUSAMBARATISHA MZIMU WA CHAMPIONS LEAGUE…

messi-suarez-neymar

Na Aidan Mlimila

Kwa mara ya kwanza vilabu vya Ulaya vilianza kushiriki mashindano ya klabu bingwa Ulaya mwaka 1955 wakati huo yakijulikana kama 'European Cup'. Yalikuwa ni mashindano ambayo yalizihusisha klabu bingwa ya kila nchi ya Ulaya na yalikuwa yakifanyika kwa mtindo wa mtoano.

Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1955 klabu ya Real Madrid ambayo ilikuwa inaongozwa na gwiji wa klabu hiyo Muargentina Alfred di Stephano ilikuwa ndiyo timu ya kwanza kutwaa taji hilo na ilifanya hivyo kwa misimu mitano mfululizo.

Kutoka kipindi hicho ambapo hayo mashindano yalikuwa yameanzishwa mpaka mwishoni mwa miaka ya 1980 ukiondoa Real Madrid kulikuwa na baadhi ya timu nyingine ambazo zilifanikiwa kutwaa taji na kuweza kulitetea. Timu kama Inter Milan, Ajax, Nottingham Forest, Benfica, huku AC Milan ikiwa timu ya mwisho kufanya hivyo.

Mwanzoni mwa miaka ya 1990 (92) shirikisho la soka barani Ulaya liliamua kuufanyia mabadiliko mfumo mzima wa mashindano hayo na ndiyo hapo ikaanza kujulikana kama UEFA Champions League mpaka leo hii.

Tokea wakati huo mpaka leo hii hakuna timu ambayo iliweza kushinda taji hilo na kulitetea msimu uliofuata. Tangu mwaka 1992 wakati ambapo mabadiliko hayo yalifanyika (reform) ni takribani miaka 24 mpaka sasa hakuna timu ambayo imefanikiwa kulitwaa na kulitetea taji la klabu bingwa ya Ulaya.

Kuna nyakati baadhi ya timu zilijaribu kufanya hivyo lakini bado ilionekana kuwa ni mfupa mgumu kwao na hapo ndipo ambapo watu wanautazama huu kama mzimu wa ile reform iliyofanyika mwaka 1992. Nakumbuka msimu wa mwaka 1995/96 kibibi kizee cha Turin Juventus ilifanikiwa kutwaa ubingwa huo wa Ulaya lakini msimu uliofuata walifanikiwa kufika hatua ya fainali lakini wakajikuta wanapoteza kwa Borusia Dortmund na hivyo kujikuta wanashindwa kulitetea taji hilo.

Msimu wa 1993/94 AC Milan walifanikiwa kutwaa taji hilo na msimu uliofuatia walipojaribu kulitetea walijikuta wakipoteza kwenye mchezo wa fainali dhidi ya Ajax.

Man Utd walifanikiwa kulitwaa kombe hilo mwaka 2008 kule Urusi lakini msimu uliofuatia walijikuta wakipoteza dhidi ya Barcelona kwenye mechi iliyochezwa kule katika uwanjani wa Olimpico jijini Roma.

Bila shaka kwa sasa unapozungumzia klabu bora kuliko zote katika bara la Ulaya kwa sasa, basi hautasita kuitaja FC Barcelona kutoka katika jimbo la Catalunya. Inapewa nafasi kubwa ya kutetea mataji yake matatu (trebble) iliyotwaa msimu uliopita.

Achana na staili yao ya uchezaji inayojulikana kama 'tik taka' ambayo asili yake ni kutoka kwa gwiji wao wazamani Johan Cruyff. Ndani yake kuna sanaa nyingine imeongezeka maarufu kama 'MSN' yaani Messi, Suarez na Neymar kwa wengine huu ni utatu mtakatifu unaoundwa na vijana watatu waliotokea katika bara la Amerika ya Kusini.

Hadi sasa wameshafunga magoli ya kutosha kwa pamoja na wamekuwa wakizifanya wanavyotaka safu za ulinzi za vilabu ambavyo wamekuwa wakikutana katika mashindano mbali mbali.

Ni juzi hapa kocha wa Arsenal mzee Arsene Wenger ameitaja MSN kama sanaa mpya kwenye soka kwa mambo ambayo wamekuwa wakifanya ndani ya mita mia moja za uwanja.

Uwepo wa MSN ndani ya kikosi cha FC Barcelona ndiyo sababu kuu inayofanya watu wazidi kuamini kuwa vijana hao wa Catalunya wana nafasi kubwa ya kuvunja mwiko na ule mzimu wa Champions League wa timu kuweza kutetea ubingwa wake, kitu ambacho kimeendelea kuwa ni mfupa mgumu kwa vilabu vya Ulaya.

Kwa ubora wa kikosi cha Barcelona na uwepo wa 'wanamazingaombwe' wale watatu kutoka Amerika ya Kusini bila shaka hauwezi kuacha kuwapa nafasi ya kulitetea taji lao.

Ni shauku ya kila mpenzi wa mchezo wa soka kuona klabu inayojitokeza kutwaa na kulitetea taji hilo kitu ambacho kimekuwa ni nadra sana kwa takribani miaka 24 sasa.

Hii siyo mara ya kwanza kwa FC Barcelona kuwa na timu bora  kwani tangu mwaka 2006 walipofanikwa kuwafunga Arsenal pale Stade de France kwenye fainali na kutwaa ubingwa ule ni takribani misimu kumi sasa na ndani ya misimu hii kumi wa-Catalunya hawa wamefanikiwa kutwaa taji hilo mara nne ikiwemo lile walilotwaa msimu uliopita pale Berlin nchini Ujerumani. Lakini mara zote hizo bado imekuwa ngumu kwao kuweza kulitetea taji hilo.

Safari ya MSN kuelekea kulitetea taji lao inaanzia kwa vijana wa Diego Simeone, Atletico Madrid baada ya draw ya robo fainali kufanyika.

Je hii sanaa mpya katika soka 'MSN' itafanikiwa kuukabili mzimu huu wa Champions League unaoishi kwa takribani miaka 24 sasa?

Bila shaka tunahitaji subira kuweza kupata majibu ya swali hili!!



Comments