MAXIMO ALIANZA, SAMATTA ANAUTOKOMEZA ZAIDI ‘U-YANGA NA U-SIMBA’ TAIFA STARS


MAXIMO ALIANZA, SAMATTA ANAUTOKOMEZA ZAIDI 'U-YANGA NA U-SIMBA' TAIFA STARS

Nahodha wa Stars Mbwana Samatta akiwa kwenye mazoezi              kuelekea mchezo dhidi ya Chad

Na Baraka Mbolembole

Mechi ya kwanza mkufunzi Mbrazil, Marcio Maximo kuishuhudia timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) ikicheza katika uwanja wa Uhuru ilimshangaza sana. Baada ya kusaini mkataba wake wa kwanza wa miaka mitatu Juni 29, 2006, Maximo alikuwa jukwaa kuu akitazama kikosi ambacho alipaswa kukichukua kutoka kwa mkufunzi 'mzalendo, Mshindo Msolla.

Stars chini ya Msolla ilikuwa ikicheza na timu ya Taifa ya Rwanda katika mchezo wa Kimataifa wa kirafiki na licha ya kwamba, Msolla aliwajumuhisha wachezaji wa klabu kubwa za Yanga SC na Simba SC katika kikosi chake cha mwisho ambacho, Maximo alipaswa kukichukua.

Kuna jambo ambalo lilikuwa ni mazoea kutokea wakati wachezaji, Victor Costa, Musa Hassan 'Mgosi', Nico Nyagawa na Ulimboka Mwakingwe wakijiandaa kuingia uwanjani kama wachezaji wa akiba.

Mashabiki waliokuwa jukwaa la upande wa kushoto kwa Maximo walianza kuzomea kwa sauti ya juu huku wakiwaambia wachezaji hao, 'hamjapendeza.'Maximo alishangazwa sana na tukio lile la mashabiki wakiwazomeam wachezaji wa timu yao ya taifa.

Kwa kuwa alikuwa Tanzania kufanya kazi ya kutengeneza timu imara ya mpira wa miguu aliulizia kwa waliokuwa karibu yake, "Kwanini mashabiki wale wanawazomea wachezaji wa timu yao ya Taifa?"

Kwanza aliambiwa kuwa, mashabiki wale ni mashabiki wa moja ya klabu mbili kubwa na zinazopendwa sana nchini. Aliambiwa kuwa wale ni mashabiki wa klabu ya Simba, na  walikuwa wakizomea kwa kuwa wachezaji wale wote walikuwa wakichezea klabu yao lakini wamevaa jezi za timu ya taifa zenye rangi za njano.

(Stars ilivaa jezi za njano zisizo na rangi nyingine yo yote ile kuanzia soksi, bukta hadi fulana ya juu, vyote vilikuwa na rangi angavu ya manjano) Baada ya kuelezwa hivyo na kuambiwa nguvu kubwa ya mashabiki hao katika mpira wa Tanzania, Maximo alitazama rangi ya njano pekee kama tatizo lake la kwanza ambalo alipaswa kushughulika nalo.

Kwa kawaida klabu ya Simba huvaa jezi zenye rangi nyekundu au nyeupe, na rangi ya njano hutumiwa na mahasimu wao Yanga hivyo kitendo cha kuwaona wachezaji wao nyota katika jezi za njano kilikuwa kikiwakera sana na kusahau kabisa kama wachezaji wale walikuwa pale kuichezea timu ya Taifa na rangi ya njano ni kati ya rangi nne zilizopo katika bendera ya Tanzania (rangi za bendera ya Tanzania ni Nyeusi, kijani, njano na bluu)

Baada ya wiki moja ya kusimamia mazoezi ya Stars kama kocha mkuu, Maximo aliitisha mechi kati ya timu ya Tanzania v Zanzibar ili kupata mchezo ambao angeutumia kuchuja wachezaji zaidi ya 30 ili kupata kikosi cha kuikabili Burkina Faso katika mchezo wa kwanza hatua ya makundi kuwania kufuzu kwa fainali za CAN 2008 nchini Ghana.

Dakika chache baada ya mechi hiyo kuanza, mashabiki wa jukwaa lilelile ambalo lilikuwa likizomea wakati wa mechi dhidi ya Rwanda, wakaanza tena kuzomea. Akiwa katika benchi, Maximo alishangazwa zaidi kwani alipowageukia kuwatazama, wakaongeza kelele za kuzomea, tena wakimuonyesha na ishara kuwa jezi walizovaa Stars hawakuzitaka siku hiyo wakicheza na Zanzibar Heroes.

Siku hiyo, Stars walivaa jezi za bluu na kijani na rangi nyeusi kwa mbali lakini kulikuwa na michirizi ya rangi ya njano katika mabega na kwapa ambayo licha ya kuwa ni midogo ili ilionekana pengine zaidi ya rangi za bluu na kijani zilizotawala katika jezi hiyo.

Maximo akaagiza kwa TFF kuwa ni lazima wapate jezi ambazo hatizakuwa na rangi ya njano kwa kuwa kufanya hivyo  wa namna yoyote ile ilikuwa ni sawa na kuwagawa mashabiki wa Stars katika pande mbili na wangeendelea kuzomewa katika uwanja wa Taifa hata dhidi ya timu ngeni katika mechi za michuano.

Stars dhidi ya Burkina Faso, Juni, 2006 kwa mara ya kwanza ilitumia jezi zisizo na rangi ya njano sehemu yo yote ile na jambo hilo nalichukulia kama sababu muhimu sana za kuvunja 'U-Simba na U-Yanga' katika timu ya Taifa Stars.

Maximo alikuja Tanzania wakati ambao mchezaji nyota na anayependwa zaidi katika timu ni yule wa kutoka Yanga ama Simba. Pamoja na kuwaridhisha mashabiki waliokuwa wakichukia uwepo wa rangi za njano katika jezi za Stars, lakini bado Maximo hakupewa sapoti ya kutosha na mashabiki wa Simba katika miaka yake minne kama kocha wa Stars.

Vikosi vingi vya kwanza vya Maximo vilikuwa na wachezaji wasiopungua 6 kutoka klabu ya Yanga, wakati ni wawili au watatu tu kutoka Simba ambao wangepata nafasi katika vikosi vyake.

Kitendo cha kuwatema waliokuwa wachezaji vipenzi wa mashabiki wa Simba wakati huo kama Juma Kaseja na Haruna Moshi kwa sababu alizodai kuwa ni za kinidhamu kilichangia sana Maximo kukosa sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki wa Simba kwa kuwa wakati huo wachezaji hao wawili walikuwa wakipendwa sana na mashabiki na walikuwa bora katika klabu yao.

Jan Borge Poulsen raia wa Denmark mara baada ya kupewa nafasi iliyokuwa imeachwa wazi na Maximo katikati ya mwaka 2010 aliwaita, Kaseja, Haruna, na wachezaji wengine waliokuwa vipenzi vya mashabiki, Athumani Idd 'Chuji,' Amir Maftah. Jan aliwaita wachezaji hao katika uteuzi wake wa kwanza wa kikosi cha Stars.

Alilenga zaidi kurudisha umoja kati ya mashabiki wa Simba na Yanga ambao walikuwa na tabia ya kushangilia timu ngeni pindi ikicheza na Stars kama tu upande fulani hautakuwa na wachezaji wa kutosha mchezoni.

Jan aliungwa mkono na kila upande kwa kuwa aliweza kuwapanga katika usawa wachezaji kutoka timu za Yanga na Simba. Hadi timu inakwenda kwa Mdenmarak mwezake Kim Poulsen mwaka mmoja baadaye tatizo la mashabiki kuizomea timu yao ya Taifa kwa sababu za kiitikadi za klabu lilikuwa limepungua.

Kim alipochukua nafasi ya Jan yeye aliwaingiza wachezaji wengi vijana, aliwapa kipaumbele wachezaji kutoka klabu hizo kubwa nchini lakini vipaji vichanga kama Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu, Frank Domayo, Shomari Kapombe, Salum Abubakary na wachezaji kama Erasto Nyoni, Aggrey Morris, Shaaban Nditti waliendelea kupata nafasi katika vikosi vyake licha ya kwambawalikuwa nje ya klabu za Yanga na Simba.

Kim kama ilivyokuwa kwa Jan hawakupata zomeazomea za kiitikadi za klabu na ni wakati wa mwalimu huyu ndipo Watanzania wameanza kuelewa kuhusu kuungana na kuisapoti Stars kwa pamoja bila kujali wachezaji wanaotumika wanatoka klabu gani.

Sasa Stars inaweza kucheza bila mchezaji ye yote wa Simba na watu wakaishangilia, sasa mchezaji nyota zaidi wa Stars kwa mashabiki si yule wa kutoka Yanga wala Simba na watu wanaishangilia kwa nguvu.

Maximo alianza, Jan akaendeleza, Kim akaboresha, wakati huu ikiwa chini ya mkufunzi mzawa, Charles Boniface Mkwassa wachezaji nyota katika timu wanatoka Tom (TP Mazembe), Samatta (KRC Genk), Kapombe, Himid Mao, Manula, Bocco (Azam FC) na bado watu wanaishangilia.



Comments