MASTAA wawili wa Barcelona, Luis Suarez na Neymar wameamua kucheza kamari wakibeti 'burger' wakati timu zao za taifa zitakapochuana katika mechi ya michuano ya kuwania kufuzu kwa Kombe la Dunia itakayopigwa Ijumaa.
Suarez mwenye umri wa miaka 29, hajacheza mechi ya mashindano akiwa na Uruguay 'La Celeste' tangu Juni 24, 2014 alipomng'ata beki wa Italia, Giorgio Chiellini na kufungiwa kucheza mechi tisa.
Straika huyo sasa amerudi kikosini na yuko tayari kumkabili Neymar – staa mwenzake Barcelona, akitarajiwa kuwa nahodha mjini Recife, Brazil.
"Nimebeti 'hamburger' na Neymar, yoyote atakayepoteza anatakiwa kulipa, bila shaka," alisema Suarez akinukuliwa na gazeti la El Mundo Deportivo. "Kila mmoja wetu ataonyesha ubora wake kwa timu yake na kiwango cha juu kwa nchi yake.
"Neymar ni mchezaji mwenzangu mzuri, mara zote tunafanya utani Barca. Juu ya yote, tu wachezaji wa timu moja na nina hakika kwamba yoyote atakayeshinda atasherehekea na yoyote atakayepoteza atafarijiwa na mwingine."
Comments
Post a Comment