PIERRE-EMERICK AUBAMEYANG wa Borussia Dortmund ya Ujerumani, amebainisha kuwa anamuheshimu sana Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp na kwamba ni yeye ndiye aliyemfanya kufikia mafanikio aliyonayo sasa.
Wawili hao walifanya kazi pamoja wakati Klopp akikinoa kikosi cha Borussia Dortmund na kufanikiwa kutengeneza urafiki wa karibu.
Staa huyo wa kimataifa wa Gabon sasa amekuwa mmoja wa washambuliaji bora katika dunia ya soka na kwa uzito mkubwa anahusishwa na uhamisho kwenda Manchester United na Arsenal.
"Klopp amenifanyia mengi," aliliambia gazeti la France Football na kufafanua kuwa kocha huyo alimjenga kitabia na kumfunza namna bora ya kuhami mchezo wake.
"Miaka miwili niliyokuwa naye ilikuwa muhimu sana na alinisaidia kukuza uchezaji wangu… ana ushawishi mkubwa na nina heshima kubwa kwa mtu huyo. Ni mmoja wa makocha watatu, pamoja na Christophe Galtier nakocha wangu wa sasa Thomas Tuchel, ambao wamenisaidia kuwa nilivyo leo," alisema.
Kauli hiyo ya Pierre-Emerick Aubameyang, yameibuka mashaka kuwa nyota huyo huenda akatua Liverpool badala ya Manchester United au Arsenal.
Comments
Post a Comment