STRAIKA nyota wa Real Madrid, Karim Benzema, ameingia kwenye ukurasa wake wa Twitter na kumjibu Waziri Mkuu wa Ufaransa, Manuel Valls aliyeshangaa uteuzi wake katika kikosi cha timu ya taifa - Les Bleus.
Mwanasiasa huyo alisema hakufikiria kama Benzema angeliitwa kuichezea Ufaransa kutokana na kashfa yake ya mkanda wa ngono.
"Mwanamichezo mkubwa anapaswa kuwa mfano kwa vijana. Mimi si Rais wa Shirikisho la Soka au Didier Deschamps. Ni juu ya kocha kuchagua timu bora iwezekanavyo, lakini nadhani kwa hali halisi si haki kwa Benzema kurudi katika kikosi cha Ufaransa.
"Soka si tu ni kwa ajili ya mashabiki. Ni ya kila mtu. Kila ishara ina athari," alisema mwanasiasa huyo akihusisha matatizo ya kisheria yanayomkabili Benzema kuhusu kesi ya mkanda wa ngono.
Akimjibu mwanasiasa huyo kupitia Twitter, Benzema aliandika: "Misimu 12 kama mtaalamu (wa soka): Nimecheza mechi 541, kadi nyekundu 0, njano 11!!! Na baadhi wanajadili kuhusu kuwa kwangu mfano wa kuigwa???"
Benzema anahusishwa na sakata hilo akidaiwa kuwa alijaribu kumshurutisha mchezaji mwenzake Mfaransa, Mathieu Valbuena kulipa pesa ili kuwanyamazisha watu waliotishia kuanika hadharani mkanda huo wa ngono.
Valbuena alikiri kuwa Benzema alipendekeza kuwa awalipe watu hao waliokuwa wakimpa vitisho ili aweze kuupata mkanda huo unaodaiwa kumuhusisha beki huyo na mpenzi wake.
Comments
Post a Comment