MWANDISHI wa filamu wa Hollywood, Adrian Butchart ana mpango wa kutengeneza filamu akiegemea kupanda kwa ajabu kwa straika wa Leicester City 'Foxes', Jamie Vardy kutoka mchangani hadi kuwa staa wa Premier League, akiweka rekodi mpya kwa kufunga katika mechi 11 mfululizo msimu huu.
Straika huyo mwenye miaka 26, anasema kwamba awali hakuweza kabisa kuelewa stori kuhusu kuwapo uwezekano wa filamu inayomhusu, alidhani ni uongo, lakini akaja kuzithibitisha baada kuzungumza na Butchart kuhusu mipango hiyo.
Vardy ameibuka na kupata umaarufu akiwa na Leicester wanaoongoza Premier League, aliojiunga nao mwaka 2012 akitokea katika klabu ya Fleetwood Town FC iliyokuwa ikishiriki ngazi ya tano ya ligi (National League) katika mfumo wa soka ya England. Sasa inashiriki League One – ligi ya daraja la tatu.
"Nilikutana naye [Butchart] na nikamuuliza kama alikuwa na wazimu... Ilikuwa katika magazeti na sikujua kama ni kweli, lakini iligeuka ilivyokuwa. Hiyo ni juu yao," alisema Vardy na kuongeza kuwa kama wanataka kufanya filamu, hakuna kitu anaweza kufanya kuwazuia.
Vardy amepiga mabao 19 katika Premier League msimu huu, akiwa nyuma ya kinara Harry Kane mwenye mabao 21 katika mbio za kuwania kiatu cha dhahabu.
Comments
Post a Comment