GWIJI wa Manchester United, Jakob "Jaap" Stam ameibuka na kueleza kwamba ndoto yake ni siku moja kuwa kocha wa timu yake hiyo ya zamani.
Muholanzi huyo ambaye kwa sasa anafanya kazi na Ajax kama kocha msaidizi baada ya kumaliza mafunzo yake ya ukocha, pia ameonyesha dalili ya kuondoka katika klabu hiyo inayoshiriki Eredivisie mara mkataba wake utakapomalizika kiangazi hiki.
"Kwanza itakuwa ni jukumu langu kufanya kazi kama kocha England, na hatimaye kama nitajiendeleza na kufanya vizuri, hakika naweza kurudi kwa kazi ya ukocha United," aliiambia Daily Mail.
Stam alisema kuwa kumekuwa na mazungumzo kwamba atamrithi Frank de Boer Ajax, lakini akasema hilo halina uhakika kwa sababu bado anagali na mkataba.
"Wanataka nibaki katika klabu, lakini wanajua lengo langu, kwamba nataka kuongoza timu ya kwanza," alisema na kuongeza kuwa tayari amewapasha Ajax kwamba anataka kujiendeleza na kwenda England, hivyo anamaliza mkataba wake kisha atasubiri hadi msimu ujao kujua kinachoendelea.
Stam aliichezea United kati ya mwaka 1998 na 2001 na kuisaidia kupata mataji matatu ya Premier League
Comments
Post a Comment