CHELSEA imepata matumaini makubwa katika mbio za kuwania saini ya Edinson Cavani baada ya wakala wa straika huyo wa Paris Saint-Germain, Fernando Guglielmone kukiri kuwa mteja wake angalipenda kufanya kazi na Antonio Conte.
Ripoti zinabainisha kuwa Conte anajiandaa kuchukua kibarua cha ukocha Stamford Bridge na inaonekana dhahiri kwamba Mtaliano huyo anaweza kuwa msaada kwa Chelsea kushinda mbio za kumuwania Cavani.
Akizungumza na Tuttosport, Guglielmone alisema: "Ndani ya miezi mitatu kila kitu kinaweza kubadilika. Edinson anaweza kukaa PSG, ambao wana mradi mkubwa, lakini pia anaweza kubadilika.
"Nani anampendelea kati ya Jose Mourinho, Conte na Massimo Allegri? Kuna makocha watatu wakubwa, lakini kwa Edy angalipendelea mchezo wa kushambulia wa Conte na Allegri."
Inaeleweka kuwa Mourinho atakuwa kocha wa Manchester United kiangazi hiki, hivyo maoni ya Guglielmone yanamaanisha kuondoa uwezekano wa Cavani kuhamia Old Trafford, huku Juventus inayonolewa na Allegri ikibaki katika mawindo ya straika huyo.
Comments
Post a Comment