CARLO ANCELOTTI anayesubiri kuanza kibarua cha kuinoa Bayern Munich mwakani akichukua nafasi ya Pep Guardiola anayekwenda Manchester City, ametoa darasa kuhusu mbinu ya kumdhibiti mwanasoka bora wa dunia, Lionel Messi asiweze kuleta madhara.
Darasa hilo alilolitoa kupitia 'kolamu' yake katika website ya Sina Sports ya China, linaweza kuwa msaada kwa makocha wengi wanaoumiza vichwa kutafuta mbinu ya kumdhibiti staa huyo anapokutana na timu zao katika mashindano mbalimbali.
Ancelotti amekabiliana na staa huyo wa Barcelona mara kadhaa wakati akiwa kocha wa Paris Saint Germain (PSG) na Real Madrid, hivyo ameona si vibaya kuwapa wengine maarifa yake na uzoefu katika kumdhibiti.
"Naweza kuwapa miongozo kama kocha. Kumkaba bega kwa bega ni ngumu sana, yeyote anayemkaba ni lazima afanye kazi hiyo kwa kiwango kikubwa sana. Njia bora ya kumzuia Messi ihusishe juhudi kubwa ya timu nzima," alieleza Ancelotti na kuongeza kuwa ni lazima kupunguza umbali kati ya kila mchezaji na kuepuka asipate mpira.
Ancelotti alisema sambamba na hilo, inahitajika pia 'kuua' eneo la kiungo la Barca: "Ni muhimu kuweka wachezaji wengi katika eneo hilo kuharibu mchezo wao katikati; unahitaji kuwazuia kufurahia uhuru wa kucheza mchezo wao wa pasi.
"Kwa kufanya hivyo, pia utakuwa umepunguza uwezekano wa Messi kupokea mpira kwa kumuweka mbali na nafasi ambazo hutumia kuleta madhara makubwa. Timu inahitaji umoja, umakini na kutoruhusu hata kufanya makosa madogo."
"Tunajua kwamba (Messi) anapenda kujitengenezea nafasi kwa kuingia eneo la hatari akitokea pembeni; wachezaji wa kiungo wanahitajika kulazimisha mchezo ili kumpa wakati mgumu wa kutengeneza nafasi ya kukimbilia ndani na kujaribu kumzima wakati akiwa pembeni kwa sababu akiwa katikati na karibu na eneo la penalty, anakuwa hana papara na anamaliza kwa kufyatua shuti la mguu wake wa kushoto."
Hata hivyo, Ancelotti anatoa angalizo kwamba unaweza kufanikiwa kumkamata Messi, lakini bado ukawa umetengeneza tatizo jingine kwa sababu Barca ina silaha nyingine katika ghala lake.
"Kama utaweka umakini wako wote juu ya Messi, unatengeneza hatari ya kutowachunga washambuliaji wengine. Ndiyo maana ninasema, inahitajika juhudi ya timu nzima wakati wowote unapocheza dhidi ya Barcelona.
"Hitimisho langu ni kwamba wakati Messi anapokuwa katika ubora wake kwa asilimia 100 katika utimamu wa kimwili, kujaribu kumzuia ni kazi bure, ni vigumu – bila kujali kocha, mbinu au mkakati wa kujihami. Kipaji kikubwa alichonacho, huwatuliza wapinzani wake kutokana na maamuzi yake ya haraka ya anachowaza kufanya. Na kama ni hivyo, hakuna njia ya kumdhibiti," alisema.
Comments
Post a Comment