REAL MADRID SASA WAMTAKA THIBAUT COURTOIS


REAL MADRID SASA WAMTAKA THIBAUT COURTOIS

MIAMBA ya soka nchini Hispania, Real Madrid sasa inataka kumsajili kipa nyota wa Chelsea ya Uingereza, Thibaut Courtois kama chaguo mbadala baada ya Manchester United kukataa kumruhusu kipa wake David de Gea kujiunga na miamba hao.

De Gea alikuwa amekaribia kabisa kuhamia Santiago Bernabeu lakini Manchester United wakatumia mbinu za kivita kukwamisha uhamisho huo katika dakika za mwisho kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili mwisho wa msimu uliopita.

Ingawaje Real Madrid wamekuwa na imani kubwa na kipa wao, Keylor Navas, lakini wanaona wazi kwamba akiumia kipa huyo au kupata tatizo, nafasi hiyo inakuwa kama haina mwenyewe.

Hata hivyo, Chelsea yenyewe haijasema kama inamuuza Courtois ingawaje kuna habari kwamba matajiri hawana kipingamizi pale inapothibitika kuna pesa ya maana mezani.
 
Kipa huyo wa kimataifa raia wa Ubelgiji amewahi kuisaidia sana Atletico Madrid mpaka kutwaa taji la Klabu Bingwa Hispania msimu wa 2013/14 ambapo Real Madrid walimmezea matae lakini wakashindwa kumsajili.


Comments