EZEQUIEL Lavezzi anayehangaikia namba katika kikosi cha Paris St-Germain (PSG) chini ya kocha Laurent Blanc, amekubali dili kubwa la mshahara wa pauni 400,000 kwa wiki kuichezea klabu ya Hebei China Fortune.
Kwa mujibu wa gazeti la Times wawakilishi wa straika huyo raia wa Argentina mwenye umri wa miaka 31, walikuwa katika mazungumzo na Chelsea mwezi uliopita, lakini dili la kutua Stamford Bridge bado halijatoa matunda na badala yake amekubali kwenda China.
Lavezzi atakuwa nje ya mkataba Paris St-Germain mwisho wa msimu huu na Hebei China Fortune iliyopanda kucheza Ligi Kuu ya China msimu uliopita, imelipa pauni milioni 3.5 kumtia mikononi.
Klabu hiyo kupitia akaunti yake ya Weibo imetangaza kufanikisha dili hilo na kutamba kuwa kuwasili kwa Lavezzi kutaifanya kuwa na fowadi kiwembe.
Comments
Post a Comment