Siku chache baada ya Simba kupokea kichapo cha bao 2-0 kutoka kwa Yanga kwenye mchezo wa VPL, kocha wa timu ya Simba Jackson Mayanja amefunguka na kusema kilichosababisha timu yake kushindwa kuibuka na ushindi kwenye mchezo dhidi ya wapinzani wao kwenye soka la Bongo.
"Vitu tulivyovifanyia mazoezi wakati wa maandalizi na plan ya mechi dhidi ya Yanga, wachezaji wangu walifanya tofauti. Lakini wangecheza kama vile tulivyokuwa tumeelekezana wakati wa mazoezi nafikiri tungefanya vizuri", anafafanua kocha huyo ambaye amepoteza mchezo wa kwanza kati ya saba tangu atue Simba.
"Watu wanaosema kwamba nilikosea kumpanga Kiiza mbele ya beki mrefu kama Bossou inawezekana hawajui kabisa mpira, ingekuwa hivyo basi akina Maradona na Messi wasingecheza soka. Kiiza sio mara ya kwanza kucheza mbele ya mabeki warefu ameshacheza mechi nyingi za kimataifa mbele ya wanigeria na wasenegal na akawafunga. Lakini wakumbukuke kuwa Kiiza ndiyo anaongoza kwa kufunga kwenye ligi hadi sasa".
"Lakini kwasababu tumepoteza mchezo kila mtu anaongea la kwake lakini mimi sitaki kusema mambo mengi ya kiufundi zaidi ila wachezaji hawakucheza kama tulivyofanya mazoezi kabla ya mchezo dhidi ya Yanga".
"Ligi bado, mechi ya Yanga siyo mechi pekee ya ligi. Sasahivi tunajipanga kwa ajili ya mechi zijazo za ligi pamoja na FA tuone tutaifikisha wapi Simba.
"Nawashukuru mashabiki wote wa Simba waliojitokeza kuishangilia timu yao, nawaomba wasikate tamaa kwasababu hii ni timu yao", anamaliza kocha huyo wa kiganda.
Mchezo ujao wa ligi Simba itakutana na Mbeya City March 6, 2016 mchezo ambao utapigwa kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam.
Comments
Post a Comment