KIUNGO wa Manchester United, Juan Mata ameeleza kilichowafanya wapate ushindi wa mabao 3 – 0 wakiwa ugenini dhidi ya Shrewsbury Town katika mechi ya raundi ya tano ya Kombe la FA akisema kwamba ni nidhamu waliyokuwa nayo.
Hata hivyo Man United walikuwa wakitarajiwa kushinda mechi hiyo licha ya kuonyesha kiwango kibovu katika wiki za hivi karibuni na Mata anapongeza kuona timu yake ikiondoka na ushindi huo mnono uliowafanya waendelee kuwepo kwenye mashindano hayo ambapo katika hatua ya robo fainali watakutana na West Ham.
"Nadhani ni mashindano maalum ya kucheza," staa huyo alikiambia kituo cha televisheni cha MUTV. "Yana historia kubwa na mechi ngumu nyingi za kucheza kama hii na nmadhani tulifanya vizuri tangu mwanzo na hiyo ndio sababu kubwa ya ushindi."
Alisema kwamba hawakuwaruhusu wapinzani wao wawasogelee na kutengeneza nafasi tangu mwanzo wa mchezo huo, jambo ambalo alisema kuwa ni zuri.
Muhispania huyo alikwenda mbali akisema kuwa, kuna baadhi ya vitu walivifanyia kazi kutokana na kuwa nyuma walikuwa wakitumia wachezaji watano, lakini akasema kwamba jambo la muhimu katika mchezo ni nidhamu na kwamba kama uko tayari kwa ajili ya mapambano basi unaweza kushinda.
Comments
Post a Comment