LUIS SUAREZ ADAI HAJUTII KUTOJIUNGA NA ARSENAL



LUIS SUAREZ ADAI HAJUTII KUTOJIUNGA NA ARSENAL

STAA wa Barcelona, Luis Suarez amesema kwamba hana cha kujutia kwa kushindwa kujiunga na Arsenal wakati alipokuwa akikipiga Liverpool.
 
Majira ya joto mwaka 2013, Arsenal walituma ofa wakimtaka Suarez lakini Liverpool walikataa kumuuza raia huyo wa Uruguay kwa mahasimu wao.

Katika msimu huo, Suarez alipata mafanikio makubwa kwa kufunga mabao 31 na kuifanya Liverpool ikaribie kutwaa ubingwa wa michuano ya Ligi Kuu.

Baada ya kupata mafanikio hayo, staa huyo mwenye umri wa miaka 29 alikwenda kujiunga na Barcelona na ameshatoa mchango mkubwa ulioiwezesha timu hiyo ya Camp Nou msimu uliopita kutwaa mataji matatu ya Ligi ya La Liga, Klabu Bingwa Ulaya na Kombe la Kopa del Rey.

Usiku wa kuamkia leo, Suarez na Barca walikuwa wageni kwenye klabu hiyo ya Emirates katika mechi ya kwanza ya michuano ya Klabu Bingwa Ulaya hatua ya 16 bora na straika huyo ambaye yupo kwenye ubora wake na ambaye msimu huu ameshafunga mabao 41 katika mashindano yote, anasema kwamba haoni cha kujutia kwa kutosajiliwa na Arsene Wenger.

"Ni jambo la kushangaza kwa watu kuzungumzia kwamba walijaribu kunisaliti wakati wanakabiliana nao katika michuano ya Ulaya," Suarez aliliambia gazeti la Daily Express.

"Ni klabu kubwa, lakini ingekuwa vigumu kucheza klabu nyingine nchini Uingereza zaidi ya Liverpool," aliongeza straika huyo.
 
Alisema kwamba Barcelona ndio lilikuwa chaguo bora kwake na akasema kuwa licha ya kufanikiwa kutwaa mataji matatu katika msimu wake wa kwanza, lakini familia yake inafurahi kuishi katika mji huo huku akisisitiza kuwa klabu hiyo ndio chaguo lake pekee kwake na maisha yanakwenda vizuri.


Comments