KOLO TOURE amesema atafanya kila awezalo dimbani kumlazimisha Kocha Jurgen Klopp kubadili mawazo juu yake na kumuongeza mkataba wa kubaki Anfield baada ya kumsajili Joel Matip.
Beki huyo raia wa Ivory Coast atakuwa nje ya mkataba Liverpool mwisho wa msimu, na tayari Klopp amekamilisha dili la usajili huru kwa Matip kutoka Schalke 04 ya Ujerumani ambaye atatua Anfield kiangazi hiki.
Dili hilo la Matip limemtia presha zaidi Toure ambaye hajapewa ofa ya mkataba mpya, ingawa beki huyo mkongwe mwenye miaka 34 ameahidi kupambana.
"Bado sina ofa yoyote kwa msimu ujao, lakini kama nitaendelea kucheza katika kiwango cha sasa, nina hakika milango itafunguliwa. Mimi ni mpambanaji," alisema Toure.
"Nipo katika timu wakati huu na ninaonyesha katika kila mechi kwamba bado nipo hapa. Haijalishi watu wengine wanasema nini, nina tabasamu hili, nina furaha sana na mara zote najitoa kwa asilimia 100 kwa klabu hii. Klabu hii ni ya ajabu. Mashabiki wananipenda.
"Kama nitaendelea kubaki katika kiwango hiki, nitalazimisha watu kubadili mawazo yao. Wakati mwingine unaweza kuwafanya watu wabadili mawazo kwa kufanya vizuri na hiyo ndiyo changamoto yangu kwa sasa.
"Naweza kuwaonyesha watu kwa mchezo wangu, kwamba bado ni mchezaji mkubwa. Hayo ndiyo naweza kufanya na nitapambana hadi mwisho."
Toure amefaidika na kuwapo majeruhi kwa Dejan Lovren, Martin Skrtelna Mamadou Sakho na amecheza mechi 16 msimu huu.
Comments
Post a Comment