GAZETI la michezo la Italia, La Gazzetta            dello Sport, limeripoti kuwa Chelsea imefikia makubaliano ya            awali na kocha Mtaliano, Antonio Conte kuchukua nafasi ya Guus            Hiddink kiangazi hiki.
        Conte mwenye umri wa miaka 46 kwa sasa ni            kocha wa timu ya taifa ya Italia, lakini kwa mujibu wa La            Gazzetta dello Sport, anatarajiwa kwa kiasi kikubwa kuachia            ngazi wakati mkataba wake utakapofika ukomo baada ya michuano            ya Euro 2016.
        Safari ya kiungo huyo wa zamani wa            Juventus kwenda Premier League itamfanya kuwa kazi yake ya            kwanza nje ya Italia.
        Huko nyuma, Conte aliajiriwa na klabu            mbalimbali za Serie A zikiwamo Atalanta, Siena na Juve kabla            ya kuchukua kazi ya kukinoa kikosi cha Italia – Azzurri            mikononi mwa Cesare Prandelli na kukiwezesha kufuzu kwa Euro            2016 bila kupoteza mchezo.
        Wakati La Gazzetta dello Sport likiripoti            kufikiwa kwa makubaliano ya awali, Express Sport linabainisha            kuwa Diego Simeone, Jorge Sampaoli na Massimiliano Allegri pia            wapo kwenye foleni ya kuingia Stamford Bridge kumbadili            Hiddink anayeiongoza Chelsea kwa muda.
        
Comments
Post a Comment