ILKAY GUNDOGAN WA BORUSSIA DORTMUND ‘KUTUA’ MANCHESTER CITY


ILKAY GUNDOGAN WA BORUSSIA DORTMUND 'KUTUA' MANCHESTER CITY

MANCHESTER City inapewa nafasi kubwa ya kuzipiga kumbo Barcelona na Juventus katika mbio za kuwania saini ya kiungo wa Borussia Dortmund, Ilkay Gundogan.

Mkataba wa staa huyo mwenye miaka 25 utafikia mwisho Westfalenstadion mwishoni mwa mwaka 2017, lakini kwa mujibu wa gazeti la SPORT, tayari ameipasha Dortmund kwamba atajiunga na City kiangazi hiki.

Kocha ajaye Etihad, Pep Guardiola, anataka mchezaji wa kiungo kuwa usajili wake wa kwanza, na inaonekana kwamba turufu yake itaangukia kwa Gundogan.

Kwa kupika mabao mawili na kufunga moja katika mechi 20 za Bundesliga msimu huu, mashabiki wa City wana matumaini kwamba kiungo huyo wa kimataifa wa Ujerumani anaweza kuwa bora zaidi kama ilivyo kwa Fernando na Fernandinho katika dimba la kati.


Comments