MANCHESTER United walikataa kufungua mlango kwa kiungo nyota wa Bayern Munich raia wa Chile, Arturo Vidal, hali ambayo imewapa mwanya Chelsea kufanya mazungumzo nae.
Meneja wa Ufundi wa Chelsea, Michael Emenalo amelazimika kusafiri hadi Italia kuangalia pambano kati ya Bayern Munich dhidi ya Juventus ambalo limemalizika kwa sare ya mabao 2-2, pamoja na mambo mengine kuangalia uwezo wa mwanasoka huyo na kuongea nae.
Mchezaji mwenyewe alipoulizwa kuhusiana na madai hayo, amejibu kwa kifupi tu akisema, "Ndio, kuna uwezekano mkubwa wa kucheza Uingereza."
Vidal alijiunga na Bayern mwezi Julai mwaka jana kwa dau la pauni mil. 25 na amekuwa akifanya mambo makubwa katika Ligi Kuu ya Ujerumani, Bundesliga.
Manchester United walishindwa kumsajili Vidal msimu uliopita na kulikuwa na fununu kwamba bosi mmoja katika klabu hiyo hakupendezwa na mwanasoka huyo kutoka Chile.
Alipoulizwa kuhusu skendo hiyo, mchezaji huyo amesema kuwa ni kweli kulikuwa na fursa ya kujiunga Man United lakini kuna mambo yalishindikana katika dakika za lala salama.
"Nilipenda ofa yao ya kwenda kujiunga na Man United lakini katika kutafuta mahali salama na pazuri zaidi kwangu, niliamua kuja Bayern. Nafikiri uamuzi wangu ulikuwa sahihi kabisa, ingawaje sasa naona kuna haja ya kupanua wigo zaidi kiuchezaji kwenda London," amesema.
Comments
Post a Comment