KIUNGO wa Chelsea, John Obi Mikel amesema kwamba asilimia 99 ya wachezaji wa klabu hiyo wanataka kocha wao, Guus Hiddink awe kocha wao wa kudumu.
Mholanzi huyo alichaguliwa kama kocha wa muda tangu Desemba mwaka jana, baada ya kufukuzwa aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Jose Mourinho, lakini licha ya kuonekana kuirejesha katika kiwango timu hiyo, amesema atastaafu majira haya ya joto.
Hii ni mara ya pili kwa Hiddink kupewa ukocha wa muda katika timu hiyo ya Blues ambapo mwaka 2009 aliiwezesha kutwaa ubingwa wa michuano ya Kombe la FA.
Kwa sasa kocha wa Atletico Madrid, Diego Simeone na timu ya taifa ya Italia, Antonio Conte ndio wanaohusishwa kukabidhiwa mikoba ya kuinoa Chelsea, lakini Mikel anasema kwamba kocha huyo wa sasa ndiye mbadala wa kuendelea kuinoa timu hiyo.
"Ni chaguo la mmiliki, klabu na bodi. Ndio watakaoamua, lakini utakapozungumzia wachezaji, kati ya asilimia 98 ama 99 miongoni mwao wanataka abaki kutokana na kwamba tunafurahi, tunafanya vizuri na tunataka jambo hilo liendelee," alisema staa huyo raia wa Nigeria.
"Ila itategemea na bodi, itategemea na Guus endapo atataka kuendelea na kazi. Ameshasema atakuwa hapa hadi mwisho wa msimu huu, lakini huwezi jua pengine anaweza kubadili mawazo," aliongea kiungo huyo.
Comments
Post a Comment