YANGA YAZIDI KUPAA, TAMBWE HAKAMATIKI



YANGA YAZIDI KUPAA, TAMBWE HAKAMATIKI
Mshambuliaji wa Yanga Amis Tambwe (katikati)              akipongezwa na wachezaji wenzake Mwinyi Haji (nyuma) pamoja              na Deus Kaseke
Mshambuliaji wa Yanga Amis Tambwe (katikati) akipongezwa na wachezaji wenzake Mwinyi Haji (nyuma) pamoja na Deus Kaseke

Hamisi Tambwe ameendeleza kasi yake ya ufungaji mara baada ya leo kutupia bao mbili nyavuni wakati Yanga ikichomoza na ushindi wa bao 3-0 dhidi ya Mbeya City kwenye mchezo wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa taifa.

Tambwe alianza kupasia nyavu kipindi cha kwanza akiutendea haki mpira uliopigwa na Simon Msuva ambaye alimzidi mbio beki wa kushoto wa Mbeya City Hassan Mwasapili kisha kuachia krosi ambayo ilimkuta Tambwe akapachika mpira wavuni.

Kipindi cha kwanza kilimalizika huku Yanga wakiwa mbele kwa bao 1-0 dhidi ya Mbeya City ambao muda mwingi wa kipindi cha kwanza walicheza kwa tahadhari kubwa huku kukiwepo na matukio kadhaa ya kuchelewesha muda.

Kipindi cha pili Tambwe akapachika bao lake la pili kwenye mchezo huo akiunganisha krosi kwa kichwa na mpira huo kumshinda mlinda mlango wa Mbeya City Juma Kaseja kisha kutinga wavuni.

Mbeya City walipata pigo kufuatia beki wao mpya waliyemsajili katika kipindi cha dirisha dogo kutoka Coastal Union Tumba Sued aliyeoneshwa kadi nyekundu na mwamuzi wa mchezo huo Jeonesia Rukyaa baada ya kumfanyia madhambi striker wa Yanga Donald Ngoma.

Thaban Kamusoko alihitimisha sherehe kwa upande wa Yanga kwa kupiga kamba ya tatu na kuipa Yanga ushindi wa bao 3-0 ikiwa kwenye uwanja wake wa nyumbani.

Kipindi cha pili mchezo huo ulijawa na vurumai za hapa na pale kutokana na wachezaji wa timu zote kutunishiana misuli na kumpa kazi ya ziada mwamuzi kazi ya ziada kuumudu mchezo huo.

Magoli mawili yaliyofungwa na Tambwe le , yanamfanya aongoze orodha ya wafungaji bora kwa kufikisha magoli 10 akimpiku striker wa Stand United Elius Maguli mwenye bao tisa hadi sasa.

Ikumbukwe Tambwe alikuwa na magoli nane kabla ya mchezo wa leo ambapo kwenye mchezo uliopita alifunga magoli matatu (hat-triki) dhidi ya Stand United na kujivuta kutoka kwenye magoli matano hadi nane.



Comments