Kuna matukio mengi sana yalitokea jana wakati wa mchezo kati ya Yanga dhidi ya Mbeya City, inawezekana ukawa hujui baadhi ya mambo yaliyojiri kwenye mchezo huo.
Shaffihdauda.co.tz imekukusanyia matukio matano ambayo yalitokea kwenye mchezo huo ambayo kwa namna moja au nyingine ulikuwa huyajui au yalikupita.
5. Jezi yenye namba kubwa kuliko zote uwanjani
Golikipa wa Yanga aliyedaka dhidi ya Mbeya City Deogratius Munish 'Dida' ndiye alikuwa mchezaji mwenye jezi yenye namba kubwa kuliko jezi za wachezaji wengine wote uwanjani.
Dida anavaa jezi yenye namba 30 mgongoni, nyota huyo wa wanajangwani tangua aanze kupewa nafasi ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza ameonesha uwezo mkubwa akifanikiwa kucheza mechi nne bila kuruhusu wavu wake kutikiswa.
4. Vurugu za mashabiki wa Mbeya City vs Yanga
Wakati kipindi cha pili kinaanza cha mchezo kati ya Yanga dhidi ya Mbeya City, zilizuka vurugu kati ya mashabiki wa timu hizo mbili ambapo baadhi ya mashabiki wa Yanga walikuwa wamekaa karibu na eneo ambalo lilikuwa na mashabiki wengi wa Mbeya City na kushuhudia mashabiki wa Yanga wakichezea kichapo kutoka kwa wale wa Mbeya City.
Polisi walilazimika kuingilia kati fujo hizo ambazo zilianza kupamba moto huku mashabiki wa Yanga wakizidiwa kutokana na uchache wao hivyo kujikuta wakibanwa kirahisi na kundi la mashabiki wa Mbeya City.
3. Mechi mbili kwa moja
Wakati Mbeya City ikicheza dhidi ya Yanga wakati huohuo kulikuwa na mechi nyingine kati ya Simba dhidi ya Yanga. Kikosi cha Mbeya City kilikuwa na wachezajin wa wanne ambao waliwahi kucheza Simba kwa nyakati tofauti hivyo walikuwa wanakutana na Yanga wakati wakiwa Mbeya City.
Wachezaji hao ni Juma Kaseja, Haruna Moshi 'Boban', Ramadhani Chombo 'Regondo' na Haruna Shamte ambao wote walianza kwenye kikosi cha kwanza cha Mbeya City.
2. Yanga vs Mbeya City iliwarudisha nyumbani Kaseke, Mwambusi na Nonga
Kocha msaidizi wa Yanga Juma Mwambusi aliwangoza wachezaji wake Deus Kaseke na Paul Nonga ambao amewahi kuwafundisha akiwa na kikiosi cha Mbeya City walikuwa wanacheza dhidi ya timu yao ya zamani ya Mbeya City ambayo waliwahi kuitumikia siku za nyuma.
Kwa upande wa Mbeya City, Juma Kaseja ni mchezaji pekee ambaye aliwahi kucheza Yanga kabla hajajiunga na Mbeya City.
1. Tambwe kuongoza orodha ya wafungaji bora
Baada ya kupiga bao mbili kwenye mchezo wa jana dhidi ya Mbeya City mshambuliaji wa Yanga Amis Tambwe alifikisha magoli 10 na kushika usukani wa orodha ya wafungaji bora wa ligi kuu Tanzania bara hadi sasa akifatiwa na Maguli mwenye magoli tisa na Donald Ngoma wa Yanga mwenye bao nane.
Comments
Post a Comment