Hizi ni habari nne zinazosumbua kwa sasa kuhusu usajili kwa vilabu vya soka vya Ulaya kwenye kipindi cha dirisha dogo la usajili mwezi January.
Manchester United wako tayari kutumia kiasi cha pauni milioni 50 (£50m) kwa ajili ya kumnasa mshambuliaji wa Tottenham Harry Kane, Chelsea nao wanamuwinda Antoine Griezmann, David Moyes kuchukua mikoba ya Gary Monk kama kocha wa Swansea na Arsene Wenger kumsaini kiungo wa kibrazil Lucas Moura.
4. Arsenal kumsajili kiungo wa Brazil
Inaripotiwa Arsenal wanajiandaa kumsajili winger wa Paris St-Germain Lucas Moura na wako tayari kutoa dau la pauni milioni 30 kwa ajili ya mbrazil huyo (BBC).
Mchezaji huyo mwenye miaka 23 amekuwa pia akihusishwa na Manchester United lakini ripoti zinasema kwamba, Arsena Wenger ameshawapiku 'mashetani wekundu' kwenye dili hilo.
3. David Moyes kuchukua nafasi ya Garry Monk kama kocha mpya wa Swansea City
Swansea City wako tayari kumpa offer David Moyes kurejea kwenye Premier Leaue kwa kumpa nafasi kocha huyo wa zamani wa Manchester United na Everton za England kuchukua nafasi ya kocha wa sasa wa timu hiyo Garry Monk.
Swansea ilichezea kipigo cha bao 3-0 kwenye uwanja wake wa nyumbani dhidi ya Leicester City siku ya Jumamosi na kupoteza mchezo wa nne ndani ya mechi tano huku wakiwa wameshinda mchezo mmoja kati ya 12 ya mashindano yote tangu August 30.
Kwa mujibu wa gazeti la The Mirror, kipigo cha Jumamosi kitakuwa ni cha mwisho kwa mwenyekiti wa timu hiyo Huw Jenkins kuendelea kumvumilia Monk.
Ripoti zinadai kwamba, Jenkins atamsaini Moyes ambaye hivi karibuni alitimuliwa na klabu ya Real Sociedad ya Hispania.
2. Forward wa Atletico Madrid Antoine Griezmann kutua Chelsea January
Chelsea inaripotiwa kumnyatia mshambuliaji wa Atletico Madrid na Ufaransa Antoine Griezmann wakihitaji huduma yake kwenye kipindi cha dirisha dogo la usajili la mwezi January.
Kikosi cha Mourinho kilichochezea kibano cha bao 1-0 kutoka kwa timu iliyopanda daraja msimu huu Bournemouth, kinahitaji kuongeza nguvu kwenye safu yake ya ushambuliaji.
Kichapo hicho kiliiacha Chelsea na maumivu ya kupoteza mchezo wa nane tangu kuanza kwa ligi msimu huu.
Kwa mujibu wa gazeti la The Mirror, The Special One yuko makini kuimarisha kikosi chake hasa safu ya ushambuliaji kwa kumdondosha Griezmann ambaye ameshafunga magoli 12 kati ya michezo 23 ya klabu yake na timu ya taifa kwenye msimu huu.
1. Manchester United wametenga kiasi cha pauni milioni 50 kumnasa Harry Kane mwezi January
Manchester United wanajiandaa kupeleka dau la pauni milioni 50 kwa ajili ya striker wa Tottenham Hotspur Harry Kane wakati wa uhamisho wa dirisha dogo mwezi January wakiwa wanatafuta suluhisho la ufungaji magoli kwenye kikosi hicho, kwa mujibu wa ripoti.
United imeshindwa kufunga goli mara saba ndani ya msimu huu wakati huo wakiwa wameng'ang'aniwa na West Ham United na kulazimishwa sare ya 0-0 kwenye mchezo wa Jumamosi uliochezwa kwenye uwanja wa Old Trafford matokeo yaliyofanya washuke hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi ya England.
Kwa mujibu wa Daily Star, Manchester United wanamuwinda Harry Kane kama mchezaji pekee ambaye watawekeza nguvu kubwa kwake na tayari wamesha tenga kiasi cha pauni milioni 50 kwa ajili ya mchezaji huyo wa timu ya taifa ya England mwenye miaka 22 ambaye ameshafunga magoli tisa kwenye mechi nane za mwisho alizocheza.
Lakini Louis van Gaal anaangalia pia majina makubwa kama mshambuliaji wa Bayern Munich Robert Lewandowski, Cristiano Ronaldo na Gareth Bale wa Real Madrid, mfungaji anayeongoza kwa magoli kwenye ligi ya EPL Jamie Vardy pamoja na winga wa Southampton Sadio Mane.
Comments
Post a Comment