POLE MOURINHO, LABDA ANGEKUWEPO TRUMAN..


POLE MOURINHO, LABDA ANGEKUWEPO TRUMAN..

mour

Nilikuwa natizama mchezo wa Chelsea dhidi ya Sunderland,  huu ulitoa picha kamili ya nini kimeendelea pale katika klabu ya Chelsea. Mashabiki walitoa ya moyoni,  wachezaji wakaonyesha walichokuwa wanataka.  Kulikuwa na mgomo wa kisekondari,  njaa zinawauma kisha mnagoma kula.

Mourinho alikuwa adui wa vijana wake mwenyewe na alikuwa malaika wa mashabiki wa Chelsea. Aliyetakiwa kuamua mchezo ni huyu mzee jeuri wa Kirusi, Roman Abramovich. Takribani mabango matatu uwanjani yalitamka ujumbe mmoja,  bango refu la rangi nyeupe na maandishi ya bluu lilisema Ukimwangusha Jose, Umetuangusha sisi.

jose1

Chini yake ambapo huwekwa bango maarufu la Terry, Lampard au Drogba lilisomeka bango la bluu lenye maana ya Jose Mourinho ni mmoja wetu na upande mmoja alisimama mtu mwenye bango la Panya watatu, Hazard,  Cesc na Costa.  Hata yalipotajwa majina yao uwanja ulizomea. Mourinho hakuwa Villas Boas, huyu ni mwokozi wa mashabiki wa Chelsea hata Benitez asingesubirishwa hivi.

Tatizo kubwa sana katika soka ni kuwa kocha huwa ndiye mhanga. Anaajiriwa ili afukuzwe, anaitwa meneja ili aweze kuwaweka sawa wachezaji. Kukitokea mgomo au matatizo maana yake Kuna dosari katika mwenendo wako. Wakati kukiwa na mgomo wa wachezaji watatu ambao ndio mastaa wa timu ni dhahiri kisu kitamwangukia mwalimu. Matajiri huamini furaha ya mashabiki ni ushindi na vikombe.

jose2

 

Huu ndio mwongozo wa kuendesha timu yoyote,  hakuna malaika kwa tajiri wa timu,  hakuna mfalme kumzidi tajiri. Kabla ya furaha ya mashabiki Kuna faida ya mwekezaji,  na kabla ya kocha Kuna wachezaji. Hizi ni sababu tatu ambazo hazimweki salama hata Pep Guardiola au hata Alex Ferguson kama hasingepata matokeo katika kipindi hiki ambacho Stoke City inaweza kununuliwa Muda wowote na mwarabu.

Na ndio maana Abramovich alihitaji mafundo mawili tu ya pombe ya Ciroc kuondoa aibu za kumtimua. Wala hakuhitaji kujali wale panya watatu kwani ndio walimpa ubingwa msimu uliopita. Mourinho atabaki katika vitabu,  atabaki kama shujaa na atabaki kama mtu aliyeipenda Chelsea.

abra

Ataishi kwenye mioyo ya mashabiki, atakaa akilini kwa Abramovich lakini ilibidi ili litokee ili maandiko yatimie. Maandiko ya maisha ya soka la Chelsea. Hakuna namna Chelsea inatakiwa kuwa Liverpool,  na hakuna namna Chelsea inatakiwa kukaribiana na Tottenham.  Ilibidi auwawe malaika Mourinho ili maadui watatu wenye nguvu waungane na timu upya.

Hata yeye Mourinho analitambua hilo,  anajua hajafukuzwa kwa roho mbaya kama wakati uliopita lakini kafukuzwa ili maisha yaendelee,  kafukuzwa kwa Upendo.  Msingi wa pesa ya Sasa unakana suala Zima la urafiki.

Msingi wa soka la Sasa umeweka urafiki na kufukuzwa makocha ndio maana sio ajabu baada ya Arsène Wenger yule kocha wa Everton, Roberto Martinez aliyeichukua timu mwaka aliofariki Mzee Mandela anafuatia kwa ukongwe ndani ya klabu moja.Hata mashabiki waliokuwa na mabango uwanjani waliyashika kwa shingo upande. Waliyashika kwa namna ya kumuonyesha hayupo mwenyewe.

martinez

Lakini katika Meza zao za chakula walihitaji na kule kwenye makasino walikuwa na msongo mkubwa wa mawazo juu ya matokeo.  Chakula kilikuwa kichungu na kamari waliliwa kila kukicha. Roho ngumu ya Abramovich ndio mwokozi pekee aliyekuwa amebaki. Roho ya Kirusi, roho ya Vladimir Putin, na roho ya kina Klistchko.

Alichokifanya Mourinho msimu uliopita akina tofauti na alichokifanya Paul Tibbets kule Hiroshima. Wakati Marekani inatishiwa nyau na Japan katika vita ya pili ya Dunia, alirejesha familia yake Marekani, akachukua ndege akaipa jina la mama yake Enola Gay.

Jenerali Paul Tibbets
Jenerali Paul Tibbets
Paul Tibbets akiwa na dege lenye jina la mama yake              Enola Gay
Paul Tibbets akiwa na dege lenye jina la mama yake Enola Gay

Kisha akaenda kuangusha Atomic akaua watu zaidi ya laki moja, akaacha hasara ya milele. Watoto wakawa wanazaliwa walemavu.  Rais wa Marekani wa kipindi hicho Harry Truman akaona isiwe shida, aliporejea nchini hakuwaza mangapi mabaya yanasemwa akampa tuzo ya heshima na kila kukicha akawa anabadilishwa vyeo.

Bahati mbaya sana Mourinho alikuwa anafanya kazi na Mrusi,  mtu ambaye hajawahi kuwa na rafiki wa kudumu.  Mrusi anayependa vita ya pesa. Mrusi ambaye baada ya kuondoka Mourinho anaungana na wachezaji kwenye uwanja wa mazoezi. Nani asiyemtaka Mourinho? LVG ananuna kufukuzwa kwa Mourinho maana kumeongeza wepesi wa yeye kufukuzwa,  Man City wanajua wakimkosa Guardiola wanamnyaka huyu, usishangae hata Liverpool wakawa wanaumia kwanini walimuwahi Klopp.

Mourinho anakupa uhakika wa ubingwa katika miaka miwili tu, hana mbwembwe.  Marekani watu wa namna hii ndio wanatakiwa, Harry Truman mtu wa namna hii ndo angependa kumshuhudia, angemtunza kama alivyomtunza Paul Tibbets.  See you next time Mourinho,  niletee Zouma mwingine popote uendako ili uwakere zaidi.

Ahsanteni.

By Nicasius Coutinho Suso

 

 



Comments