Shirikisho la Mpira wa Miguu              nchini (TFF) litamfikisha kwenye Kamati ya Maadlili mapema              Mwakani baada ya sikukuu ya mwaka Mpya 2016, Mkuu wa              Mawasiliano wa klabu ya Yanga, Jerry Muro kutokana na kauli              zake za kibaguzi dhidi ya Mkuu wa Mawasiliano wa klabu ya              Simba, Haji Manara.
        Muro alimshambulia kwa maneno ya              kibaguzi Manara wakati akizungumza na Waandishi wa Habari              katika mkutano uliofanyika jana makao makuu ya klabu ya              Yanga jijini Dar es Salaam.
        Kauli ya Muro dhidi ya Manara ni              kinyume na Katiba ya TFF, Shirikisho la Mpira wa Miguu              Afrika (CAF) na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu              (FIFA) ambao zinapiga vita vitendo vya ubaguzi wa aina              yoyote katika mpira wa miguu.
        Mapema mwaka huu, Muro alifikishwa              kwenye Kamati ya Nidhamu ya TFF kutokana na kumshambulia na              kumdhalilisha kupitia vyombo vya habari aliyekuwa Kaimu              Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB),              Fatma Abdallah. Kamati ya Nidhamu ilimwadhibu kwa kumpiga              faini ya sh. milioni 5.
        
Comments
Post a Comment