Bournemouth imeichapa Manchester United 2-1 katika mchezo mkali wa Premier League, matokeo yanayozidi kumweka kocha wa United Louis van Gaal kwenye shinikizo kubwa.
Timu hiyo inayoshika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi, wiki iliyopita ilichukua pointi tatu mikononi mwa Chelsea kwa ushindi wa 1-0.
United ilicheza vizuri sehemu ya kiungo na ulinzi japo upande wa kushoto ilipwaya, lakini ni sehemu ya ushambuliaji ndiyo iliyoonekana kikwazo zaidi kwa Van Gaal.
Washambuliaji wa Manchester United walishindwa kabisa kulitia misukosuko ya maana lango la Bournemouth na hata nafasi chache zilizopatikana zilipotea kirahisi.
Bournemouth walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya pili tu ya mchezo kupitia kwa Junior Stanislas aliyepiga kona iliyokwenda moja kwa moja wavuni huku kipa David de Gea akiishia kuugusa mpira kwa ncha za vidole.
United ikapambana na kusawazisha dakika ya 24 kwa bao la kulazimisha lililotokana na juhudi binafsi za Marouane Fellaini.
Hata hivyo sikio la kufa halisikii dawa, dakika ya 54 Josh King aliyewahi kuichezea Manchester United, akaisulubu timu yake ya zamani kwa kuifungia Bournemouth bao la pili na kumsha shangwe kwenye uwanja uliokuwa na watazamani 11,334.
BOURNEMOUTH: Boruc, Smith, Francis, Cook, Daniels, Surman, Ritchie, Arter (O'Kane 86), Gosling, Stanislas, King (Murray 65)
MANCHESTER UNITED: De Gea, Varela, McNair (Jones 91), Blind, Jackson, Fellaini (Powell 74), Carrick, Mata, Depay, Lingard (Pereira 31), Martial
Mchezaji wa zamani wa Manchester United Josh King akishangilia bao lake aliloifungia Bournemouth
Wachezaji wa Bournemouth wakishangilia bao lao la kwanza lililofungwa na Junior Stanislas (katikati)
Junior Stanislas alipiga kona iliyosindikizwa kwenda wavuni na kipa wa United David de Gea
Marouane Fellaini anaisawazishia United kwenye dimba la Vitality Stadium
Fellaini akipongezwa na mchezaji mwenzake Jesse Lingard
Comments
Post a Comment