FIGISU SOKA LA BONGO: COASTAL UNION, MBEYA CITY KUPELEKANA TFF KISA MCHEZAJI HUYU


FIGISU SOKA LA BONGO: COASTAL UNION, MBEYA CITY KUPELEKANA TFF KISA MCHEZAJI HUYU

Tumba-Swed-mccfc

Figisu za usajili wa bongo tayari zimeshaanza kujitokeza baada ya dirisha dogo la usajili kufunguliwa ili vilabu kufanya usajili kwa ajili ya kuimarisha vikosi vyao katika harakati za kuhakikisha vinafanya vizuri kwenye ligi kuu Tanzania bara, ligi daraja la kwanza na ile ya daraja la pili.

Klabu ya Mbeya City imeingia katika sintofahamu dhidi ya klabu ya Coastal Union baada ya 'wagonga nyundo' wa jiji la Mbeya kumsajili beki wa kati wa Coastal Union Tumba Swed kitendo ambacho kimelalamikiwa na 'wagosi wa kaya' kwamba kuna taratibu ambazo hazikufuatwa katika kukamilisha uhamisho wa mchezaji huyo.

Kutokana na sakata hilo klabu ya Coastal Union imesema itabisha hodi kunako shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupeleka malalamiko yao juu ya timu ya Mbeya City kumsajili mchezaji wao kinyume cha taratibu.

Costal Union kupitia kwa mwenyekiti wake wa usajili Alhaj Salim Bawazir umeweka wazi msimamo wao wa kumuwekea pingamizi aliyekuwa beki wao Tumba Swed ambaye amejiunga na klabu ya Mbeya City.

Bawazir amesema Tumba ni mchezaji wao halali na ana mkataba na Coastal Union unaomalizika mwezi January 2016 hivyo watapeleka pingamizi lao TFF kwa kuitaka Mbeya City ifate taraibu za usajili.

"Tutapeleka pingamizi kwenye chama cha mpira (TFF) kwa ajili ya mchezaji Tumba Swed ambaye amechukuliwa na Mbeya City, Mbeya City walizungumza na Swed wakakubaliana sisi hatuna mushkeli yeyote kukubaliana kwao lakini kwetu sisi anamkataba ambao unamalizika mwezi January 31, 2016 kwahiyo tutapeleka pingamizi TFF kwamba Mbeya City hawakufuata utaratibu wa kuja kuzungumza na sisi", anasema Alhaj Bawazir.



Comments