Unapokuwa kocha na ukafanikiwa kushinda kila kombe ambalo umewahi kushindani kuanzia ngazi ya klabu na mpaka ngazi ya timu za taifa, ni mafanikio makubwa na hata unapoamua kustaafu baada ya hapo hakuna atakayekupinga.
Habari kutoka nchini Hispania imethibitishwa rasmi kwamba kocha wa timu ya taifa ya nchi hiyo Vicente del Bosque anatarajia kustaafu baada ya mashindano ya Euro 2016.
Kocha huyo wa zamani wa timu ya Real Madrid mwenye umri wa miaka 64 aliiongoza Spain kushinda ubingwa wa ulaya mara 2012 na kombe la dunia mwaka 2010.
"Muda wangu wa kustaafu umefika. Ikiwa kila kitu kitaenda kilivyopangwa – baada ya Euro 2016 nitastaafu," alisema Del Bosque aliyeshinda Ubingwa wa ulaya ngazi ya vilabu na Real Madrid mwanzoni mwa miaka ya 2000.
"Nitachukua maamuzi rasmi baada ya kuongea na shirikisho la soka la Hispania."
Spain walishinda ubingwa wa kwanza wa ulaya 2008 wakiwa na hayati Luis Aragones, na Del Bosque akautetea ubingwa huo 2012 na sasa kabla hajastaafu ataiongoza nchi yake kuutetea ubingwa huo nchini Ufaransa.
Kocha wa FC Barcelona Luis Enrique amesema angependa kuifundisha nchi yake wakati Del Bosque atakapostaafu lakini huenda kocha Pep Guardiola akaitaka nae nafasi hiyo baada ya jana kutangaza rasmi kwamba ataondoka Bayern Munich mwishoni mwa msimu.
Comments
Post a Comment