Biashara ya Kwanza Kati ya Wenger na Mendes Ilivyoingia Mdudu


Biashara ya Kwanza Kati ya Wenger na Mendes Ilivyoingia Mdudu

Msimu wa usajili wa wachezaji kwa vilabu vya soka barani ulaya unatarajiwa kufunguliwa rasmi mnamo January 1, 2016, na kama ilivyo kawaida vilabu mbalimbali vimeshaanza mipango ya usajili, Arsenal ni klabu mojawapo. 

 Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa na gazeti la El Confidencial, Gunners walikuwa wanasubiri dirisha lifunguliwe tu wakamilishe usajili wa mchezaji kiungo wa Atletico Madrid Saul Niguez, lakini uhamisho umekwamba kutokana na majeruhi.

El Confidencial wanaripoti kwamba wakala wa Saul, Jorge Mendes, alishakubaliana kila kitu na Arsenal lakini Atletico wameamua kusitisha dili hilo baada ya kiungo wao Tiago kuvunjika mguu katika mechi ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Espanyol, na sasa "Saul amekuwa muhimu kwa Atletico hivyo hawezi kuuzwa.

Hili ni pigo kwa Arsenal ambao walikuwa wanategemea usajili wa Saul ungeziba pengo au kupunguza makali ya kuwakosa Francis Coquelin, Jack Wilshere, Mikel Arteta Santi Cazorla walio na majeruhi.
Saul, mwenye umri wa miaka 21, ana mkataba na Rojiblancos 'Atletico Madrid' mpaka mwaka 2020.

Endapo uhamisho huu ungefanikiwa basi ingekuwa ndio mara ya kwanza kwa Arsene Wenger kufanya biashara na wakala maarufu duniani Jorge Mendes.

Huko nyuma Wenger ameshawahi kuingia kwenye malumbano na Mendes baada ya kusema kwamba:

'Mendes ana muelekeo tofauti na wangu, yeye anadili na vilabu vyake maalum. Mimi nafanya kile kilicho sahihi kwa klabu na kihalali, lakini kama nadhani ana mchezaji ambaye atakuwa muhimu kwa mahitaji ya klabu, ningependa kufanya nae biashara, ila sidhani kama itawekezekana, Mendes hajawahi kunifanyia jambo lolote la kipekee.'



Comments