ZANZIBAR HEROES YAKABIDHIWA BENDERA, AGREY MORRIS KUKOSA CHALLENGE MWAKA HUU



ZANZIBAR HEROES YAKABIDHIWA BENDERA, AGREY MORRIS KUKOSA CHALLENGE MWAKA HUU
Dr. Mwinyi Haji Makame (kulia) akimkabidhi bendera ya              Zanzibar Awadh Juma
Dr. Mwinyi Haji Makame (kulia) akimkabidhi bendera ya Zanzibar Awadh Juma

Na Abubakar Kisandu, Zanzibar

Wachezaji wa timu ya taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes)  wametakiwa kuwa na umoja, ushirikiano na nidhamu ya hali ya juu katika kipindi chote mashindano ya Challenge Cup yanatarajiwa kuanza  tarehe 21 ya mwezi huu Adis Ababa nchini Ethiopia.

Ushauri huo umetolewa na Dr. Mwinyi Haji Makame ambaye alikuwa mgeni rasmi katika shughuli nzima ya kuwaanga wachezaji hao pamoja na kuwakabidhi bendera na wimbo wa taifa la Zanzibar katika ukumbi wa VIP Amaan Unguja.

"Ushirikiano, umoja, kupendana pamoja na nidhamu ndio silaha yenu ya kufanya vizuri, lazima viongozi wenu muwasikilize na msilaumiane, mkifanya hivyo mtafanikiwa kufanya vizuri huko Ethiopia", amesema Mwinyi Haji.

Wakati huo huo Dr. Makame alimkabidhi bendera na CD ya wimbo wa taifa la Zanzibar nahodha wa timu hiyo Awadh Juma huku akimsisitiza kuwa wanawakilisha wazanzibar wote kwenye mashindano hayo ndio mana wakakabidhiwa bendera na CD.

"Nakukabidhi bendera hii na CD Captain wetu kwa heshima kubwa ya nchi yetu ili mkatuwakilishe vizuri kwani wazanzibar watakuangalieni kwenye mashindano hayo kupitia TV".

Kwa upande wake captain wa timu hiyo Awadhi Juma amewaahidi Wanazanzibar kwamba watarudi na kombe bila ya hofu yoyote kwani wao wanaenda kushindana na si kushiriki.

"Sisi tunaenda kupambana  na si kushiriki , kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu tutarudi na ubingwa kwani tunajua umuhimu wa mashindano, hivyo siku tutakayorudi mashabiki waje kutupokea kwa wingi uwanja wa ndege".

Kwa upande mwingine mlinzi wa kati Agrey Moris hatokwenda Ethiopia kutokana na majeruhi aliyokuwa nayo kufuatia mchezo wa juzi wa kirafiki kati ya Zanzibar Heroes na kombaini ya makocha baada ya kuumia na kushindwa kumaliza mchezo huo kwenye uwanja wa Amaan ambapo Heroes ilishinda 1-0 kwa bao la Khamis Mcha.

Daktari wa timu ya Zanzibar Heroes Mohamed Said Mwinyi amethibitisha kuumia Agrey na kusema kuwa atakaa nje ya uwanja zaidi ya wiki mbili na nafasi yake kocha Malale Hamsini amemchukua Shaffii Hassan mlinzi wa timu ya Zimamoto.

Tumemtafuta mlinzi huyo Shaffi aliechaguliwa kuchukua nafasi ya Agrey na kusema kuwa anafuraha sana.

"Nimefurahi kocha kuniona mimi nafaa na kunichagua, naamini nitafanya vizuri kwani mimi pia ni mzoefu katika mashindano hayo",alisema Shaffii.

Kikosi hicho kinaundwa na;

Makipa: Mwadini Ali (Azam), Mohamed Abraham (JKU).

Mabeki wa pembeni: Mwinyi Haji (Yanga), Nassor Masoud (Stand United), Adaymu Saleh (Coastal Union) na Ismail Khamis (JKU).

Walinzi wa kati: Nadir Harub (Yanga), Shafii Hassan (Zimamoto), Said Mussa (Mafunzo), Issa Haidary (JKU).

Viungo: Awadhi Juma (Simba), Mudathir Yahya (Azam), Saidi Makapu (Yanga), Mohamed Abdulirahmani Mbambi (Mafunzo), Hamis Mcha (Azam), Suleiman Kassim (Stand United) na  Omari Juma (Hard Rock).

Washambuliaji: Ibrahimu Hilika (Zimamoto), Mateo Antony (Yanga) na Ame Ali (Azam).

Kikosi cha Zanzibar Heroes kinatarajia kuondoka kesho majira ya saa 9 alaasiri kwenye uwanja wa ndege wa Abeid Aman  Karume na kitafikia  Dar es Salam na wataondoka kwenye uwanja ndege wa Dar kisha wataondoka na watatumia ndege ya Ethiopia  na kwenda moja kwa moja Ethiopia.

Mwamuzi wa Zanzibar mwenye beji ya FIFA Mfaume Ali Nassor ambaye pia kachaguliwa kwenda kuchezesha mashindano hayo tayari ameondoka visiwani leo hii akifatana na mjumbe wa kamati ya utendaji ya CECAFA Mzee Zam Ali kwenda kwenye mashindano hayo.

Zanzibar wapo kundi B pamoja na Burundi, Kenya na Uganda  na mchezo wao wa mwanzo watacheza na Burundi November 21.



Comments