KOCHA wa Arsenal, Arsene Wenger amelitupia lawama Shirikisho la Soka barani Ulaya (UEFA), kwa kuruhusu matumizi ya dawa za kuongeza nguvu baada ya kushindwa kuiadhibu Dinamo Zagreb kwa kumchezesha mchezaji ambaye anatumia dawa hizo wakati timu hizo zilipokutana mwezi uliopita.
Katika mchezo huo wa Kundi F uliopigwa Septemba 16, ambao Dinamo iliichapa Arsenal mabao 2-1, mchezaji Arijan Ademi alicheza dakika zote 90 lakini baadae alipopimwa alibainika kuwa na matumizi ya dawa hizo.
Baada ya kubainika, UEFA ilimfungia Ademi miaka minne, lakini matokeo ya mechi hiyo yameendelea kubaki hivyohivyo, kitu ambacho anakilalamikia Wenger.
"Ndio na inanishangaza kuhusu uamuzi huu. UEFA imekuwa ikitumia sheria ambazo wameziandaa lakini wamekuwa hawazitekelezi kutokana na kwamba kama kuna mchezaji amebainika kutumia dawa, lazima na matokeo yabatilishwe, lakini kama hawakufanya hivyo wanakuwa wamekubaliana na matumizi ya dawa hizo," alisema Wenger.
Alisema, kama Shirikisho hilo linakubaliana na hali hiyo, hawana jinsi bali watalazimika kuangalia kiwango chao.
Comments
Post a Comment