WANARIADHA WA KENYA WALIVYOLIANZISHA ZOGO LA KUPINGA UFISADI



WANARIADHA WA KENYA WALIVYOLIANZISHA ZOGO LA KUPINGA UFISADI
KUNDI la wanariadha waliojawa na hamaki lilivamia makao makuu ya Shirikisho la Riadha nchini Kenya (AK) na kufunga milango wakilalamikia ufisadi na ubadhilifu katika ofisi hiyo iliyopo mjini Nairobi.
Wanariadha hao waliwazuia maafisa wa Shirikisho hilo la AK kuingia ofisini mwao, huku wakiwa wamebeba mabango ya kukashifu uongozi duni na ufisadi uliokithiri ofisini humo.

Maandamano hayo yanafuatia madai ya hivi punde kuwa takriban dola laki saba za Marekani, fedha za ustawishaji wa riadha nchini Kenya ziliporwa na maafisa wakuu watatu wa shirikisho hilo.

Fedha hizo zilikuwa zimetolewa na kampuni ya kutengeneza vifaa vya michezo ya NIKE, iliyopewa zabuni ya kutengeneza sare za timu ya taifa ya riadha.

Naibu Mwenyekiti wa Shirikisho hilo, David Okeyo tayari anachunguzwa na idara ya kupambana na ufisadi, huku mwenyewe akiwa anakana madai hayo dhidi yake.

Vilevile, wanariadha hao wanalilaumu Shirikisho hilo la Atheltics Kenya kwa kupokea hongo kutoka kwa mawakala wanaoshukiwa kuwashawishi wanariadha nchini humo kutumia madawa ya kututumua misuli yaliyopigwa marufuku duniani.

Kenya ni moja ya mataifa yaliyotajwa kuwa na tatizo sugu la utumiaji wa dawa hizo za kuongezea nguvu mwilini na shirikisho la kupambana na matumizi ya dawa hizo duniani (WADA).

Afisa aliyeongoza uchunguzi wa Shirikisho la Riadha Duniani, Dick Pound alishauri WADA iangazie kurunzi yake kwenye ofisi za Shirikisho la Riadha la Kenya baada ya kuitimua Urusi.

Wanariadha hao wanadai kuwa, maafisa wa AK wamekuwa wabinafsi sana na sasa wanatishia posho zao, ambapo wanawataka waondoke ofisini na nafasi zao zichukuliwe na wanariadha wa zamani.  


Comments