Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam,
Wachezaji 6 wanataraji kutimka leo kurudi mikoani mwao, na tayari wachezaji zaidi ya 8 wameondoka kwa 'taabu'. Hakika kinachoendelea sasa ndani ya Majimaji FC ya Songea si jambo la kufurahisha hasa ukizingatia ndiyo kwanza timu hiyo imerejea katika ligi kuu msimu huu baada ya kuteremka ligi daraja la kwanza msimu wa 2010/11.
Habari za ndani kabisa ya timu hiyo ambazo nimezipata na kuthibitishwa na baadhi ya wachezaji wa timu hiyo ni kwamba, hali ya kiuchumi ndani ya Majimaji ni mbaya na wachezaji wamelalamikia utawala wao kwa madai kuwa 'upo kimaslai' na ndiyo maana wachezaji wameshindwa kurudi majumbani mwao tangu kuvunjwa kwa kambi mapema mwezi huu.
" Hali ya kiuchumi ni mbaya sana, wachezaji wanaishi kwa kutegemea misaada midogo midogo kuna kwa ndugu, jamaa na baadhi ya marafiki" anasema mmoja wa wachezaji wa timu hiyo ambaye hakuwa tayari kutajwa jina lake. " Viongozi wapo kimya, ukiwatafuta hawapatikani, ukiwapigia simu hawapokei. Wachezaji wengi wameondoka wiki iliyopita baada ya kusaidiwa na watu wao wa karibu"
Majimaji ambayo ipo chini ya kocha raia wa Finland, Mika ilianza msimu kwa ushindi wa mechi 2 mfululizo lakini mwenendo wao mzuri ulibadilika na kuwa matokeo ya kukatisha tamaa. Najiuliza tu, inakuwaje timu ina muajiri kocha kutoka barani ulaya lakini kila siku wachezaji wanalalamika ukata.?
"Matatizo haya hayajaanza sasa, yapo kitambo. Matatizo ya timu hii ni pesa tu. Viongozi wa timu wapo kimaslai sana. 'Wanapiga' sana pesa kupitia timu hii." Wachezaji wote (6) wenyeji wa Songea wamerudi majumbani kwao, wawili wa Dar, mmoja wa Iringa wameshaondoka baada ya kusaidiwa na ndugu zao. Kesho ( Leo) kuna wachezaji wengine 6 wanaondoka, mimi mwenyewe na wachezaji wengine kama 6 tunatarajia kuondoka Keshokutwa ( Kesho Jumanne)"
Comments
Post a Comment