BILA hiyana, kocha wa klabu ya Manchester United, Louis Van Gaal, ameweka wazi kuwa hivi sasa wanasafiria nyota ya shujaa wao mpya, Memphis Depay.
Van Gaal amesema, Manchester United ambayo kwa sasa inapambana kurejea katika ubora wake, inaamini winga huyo raia wa Uholanzi mwenye miaka 21, atatimiza matarajio yao.
Memphis aliyejiunga na United msimu huu akitokea PSV Eindhoven ya Uholanzi na kupewa jezi namba saba, ambayo ilikuwa ikitumiwa na mastaa waliong'ara ndani ya klabu hiyo, amethibitisha kuwa atalinda heshima ya namba hiyo.
mchezaji huyo mwenye kasi na chenga za maudhi, aliyezaliwa Februari 13, 1994 mjini Moordrecht, Uholanzi, aliigharimu United paundi mil.31.
Winga huyo aliyechezea PSV Eindhoven mechi 90 na kuifungia mabao 31 kwa miaka minne aliyodumu hapo ameonyesha matumaini makubwa Old Trafford.
Alitua United kiangazi cha mwaka huu na wengi wa mashabiki walidhani kocha Van Gaal amembeba kwasababu ni Mholanzi mwenzake.
"Kwa hakika, Depay ameonyesha uwezo mkubwa licha ya kwamba bado hana uzoefu wa kutosha, lakini ameonyesha ni mchezaji wa aina gani na sasa klabu imeweka matarajio kwake," alisema Van Gaal.
Alisema, mchezaji huyo aliyebadilishwa kutoka mchezaji wa benchi na kuwa tegemeo kwenye kikosi cha kwanza cha PSV, analizoea soka la Uingereza kwa haraka.
Mbali ya Van Gaal, mshambuliaji mahiri wa zamani wa zamani wa Liverpool, Dirk Kuyt, ameifagilia klabu hiyo akisema imelamba dume kwa kumsajili Memphis.
"Kwa muda mfupi niliofanyakazi na Memphis kwenye timu ya taifa ya Uholanzi, nimejiridhisha kuwa ni mchezaji mwenye kipaji cha hali ya juu na atakuwa staa baadae," alisema.
Amesema mchezaji huyo amekuwa hajivungi kujifunza kutoka kwa magwiji na makocha, jambo litakalomfanya kukamilika kiuchezaji.
Comments
Post a Comment